Baraza la Sanaa nchini (Basata) limefafanua umuhimu wa kibali ambacho msanii Diamond alipaswa kuwa nacho kabla ya kwenda kufanya shoo nje ya nchi.
Haya yameelezwa jana Julai 27 baada ya Diamond kuzuiwa kwa saa tisa katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere kutokana na kutokuwa na kibali hicho alipokuwa akielekea visiwa vya Madagascar na Mayote.
Kaimu Katibu Mkuu wa Basata, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Onesmo Kayanda, amesema kibali hicho kinawasaidia kutunza kumbukumbu ya wasanii wanaokwenda nje ya nchi.
Jingine ni endapo atapatwa na tatizo lolote iwe rahisi kumsaidia na kuongeza kuwa kuna baadhi yao walishakumbwa na matatizo wakiwa nje ya nchi huku serikali ikiwa haina taarifa kama walisafiri.
Kibali hicho ambacho gharama yake ni Sh50,000, Kayanda amesema huchukua siyo zaidi ya dakika 20 kukipata isipokuwa tu wasanii huzembea.
“Kuanzia sasa hivi tutakuwa wakali katika hilo bila kujali ukubwa wa jina la msanii, kwani ni kitu ambacho kipo kwenye sheria na ni kwa faida ya wasanii wenyewe na Diamond siyo wa kwanza kuzuiwa, wapo wengine labda kwa kuwa hawana umaarufu kama aliokuwa nao Diamond ndiyo maana haikuzungumzwa sana,” amesema.
Hata hivyo kibali hicho baadaye kitaisaidia serikali kujua sekta ya sanaa inachangia pato la taifa kwa kiasi gani kwa wasanii kupata shoo za nje kwani katika hatua hiyo pia watapaswa kuweka na mikataba yao mezani ya mialiko kujua serikali nayo imepata nini katika suala zima la kodi.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment