Rais John Magufuli amesema atahamia jijini Dododma kabla mwaka huu haujamalizika kama alivyoahidi serikali yake kuhamia huko.
Rais Magufuli amesema hayo wakati akizungumza katika hafla fupi ya kuwakabidhi hati za viwanja kwa mabalozi wa nchi mbalimbali na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, Ikulu jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Julai 30.
Amesema hadi sasa viongozi wengi wa serikali wameshahamia Dodoma akiwamo Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, mawaziri na viongozi mbalimbali wa kitaifa na kwamba Dar es Salaam amebaki yeye tu.
“Nimebaki mimi tu hapa. Nimepanga kabla mwaka huu haujamalizika nitahamia Dodoma, nilitaka nisihamie huko nikawaacha ndugu zangu wanaowakilisha nchi zao hapa Dar es Salaam, ndiyo mana nikahakikisha mnapata hati.
“Serikali imetoa maeneo mbalimbali jumla ya heka tano bure kwa ajili ya mabalozi, na ninyi ni mashahidi nimetoa hati hizi bila kudai chochote na mmepatiwa bila kusaini chochote, sijasema mhamie kesho, mtahamia wakati wowote mtakaotaka,” amesema Rais Magufuli.
Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli amesema, tayari viongozi wote na watumishi zaidi ya 6,000 wameshahamia hukoa ambapo pia amewatoa hofu mabalozi hao na wawakilishi wa kimataifa kuhusu usalama jijini humo.
“Tunaamini katika hatua tunazochukua mkihamia Dodoma itakuwa safi na kuhusu usalama tumehakikishiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa.
“Dodoma ni mahali pazuri na ni rahisi kwenda nchi yoyote kwa kuanzia Dodoma. Tunaboresha huduma za usafiri ikiwamo miundombinu na afya kwa Dodoma na mikoa jirani ukiwamo Singida.
“Nimeagiza ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa msalato ili ndege zinazotua Dar es Salaam zitue Dodoma uanze kujengwa mara moja. Nataka niwahakikishie mabalozi Dodoma ni mahali pazuri nina uhakika patakuwa safi sana hasa baada ya ndege kutoka nchi zenu kutua hapa, tunataka kuitengeneza Tanzania mpya, yenye maendeleo na kushirikiana na sekta binafsi,” amesema.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment