Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro, ameagizwa kumpangia kazi nyingine Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mohamed Shekhan Mohamed, kutokana na kusuasua kwa ujenzi wa nyumba 36 za polisi.
Agizo hilo lilitolewa jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni, alipofanya ukaguzi wa ujenzi wa nyumba hizo mpya za askari.
“Hatua ya kwanza namwelekeza IGP ambadilishe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba na ampangie kazi nyingine. Pili, kwa muda mfupi aje mwenyewe aangalie kinachofanyika asisubiri ripoti,” alisema.
Nyumba hizo ni zile zinazojengwa eneo la Mfikiwa, wilaya ya Chake Chake, Kusini Pemba ambazo jiwe la msingi liliwekwa Machi 20, mwaka huu, na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika eneo hilo jana, Masauni alimtaka IGP Sirro kufika Pemba ndani ya wiki mbili akajionee yanayoendelea badala ya kusubiri ripoti.
“Akija amchukue na Kamishna wasimamie ujenzi wa nyumba hizi kama nilivyotoa ahadi wakati wa kuweka jiwe la msingi mbele ya Makamu wa Rais na wakati wa uzinduzi wa nyumba Arusha uliofanywa na Rais John Magufuli,” alisema.
Wakati wa uzinduzi huo, Makamu wa Rais alimtaka IGP Sirro kuwachukulia hatua mara moja askari polisi ambao wamekiuka maadili na taratibu za jeshi katika mkoa wa Kusini Pemba.
Aidha, alilipongeza Jeshi la Polisi nchini kuhakikisha nchi inakuwa tulivu na yenye amani.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment