Mbowe Kapigwa Onyo la Mwisho na Mahakama.....Akirudia Dhamana Yake Itafutwa

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imesema itamfutia dhamana Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe endapo akishindwa kufika mahakamani bila sababu za msingi.

Hayo yamesemwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya Wakili wa serikali, Faraja Nchimbi kuhoji kwanini Mbowe hajafika mahakamani hapo mara mbili mfululizo.

Nchimbi ameeleza kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali lakini mshtakiwa wa kwanza Mbowe hayupo.

“Tunaomba mahakama itoe onyo kwa washtakiwa kuhusu kutofika mahakamani,”.

Baada ya kueleza hayo alisimama mdhamini wa Mbowe na kueleza kuwa amekwama kwenye foleni wakati akija mahakamani.

Naye wakili wa utetezi, Hekima Mwesipu amedai kuwa Mbowe amekwama katika foleni kwa sababu ya msafara wa kiongozi aliyekuwa akipita.

“Mdhamini amesema Mbowe amekwama katika foleni, hivyo angepata dharura nyingine angesema, “ Mwesipu.

Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Mashauri amesema anatoa onyo la mwisho kwa Mbowe na endapo akirudia atamfutia dhamana.

“Mdhamini ukamwambie kuwa tutamfutia dhamana, asikutumie wewe kama chambo,” amesema Hakimu Mashauri

Baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo hadi August 2,2018 kwa ajili ya usikilizwaji wa awali.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk.Vincent Mashinji na Manaibu wake, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Wengine ni Mchungaji Peter Msigwa ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini, Esther Matiko (mweka hazina wa BAWACHA), Halima Mdee (mbunge, Kawe), John Heche (mbunge, Tarime Vijijini), Ester Bulaya (mbunge, Bunda).Kwa pamoja, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 13, yakiwamo ya kufanya mikusanyiko na maandamano yasiyo halali.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo February 16, 2018 katika Barabara ya Kawawa, eneo la Kinondoni Mkwajuni na kusababisha vurugu zilizosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline.


from MPEKUZI

Comments