Lipumba Awataka Wapiga Kura Waiadhibu CCM kWa Kupandikiza Usaliti Ndani ya Chama Chake

Mwenyekiti wa CUF (anayetambuliwa na Msajili wa Vyama), Profesa Ibrahim Lipumba amewaomba wananchi wa Kata ya Nachingwea Wilaya Ruangwa mkoani Lindi, kupinga kitendo cha CCM cha kupandikiza usaliti kwenye chama chao.

Profesa Lipumba anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ameyasema hayo jana alipokuwa akimnadi mgombea wao wa udiwani, Abubakar Safi Kondo kwenye kata hiyo.

Lipumba amesema wapiga kura wilayani Ruangwa wanatakiwa kurudisha salamu kwa CCM kwa kitendo chao cha kumshawishi diwani wao kuwasaliti na kujiunga na chama hicho ambacho kimemteua kugombea tena kwenye kata hiyo.

“Lazima tulete mabadiliko, CCM wameshindwa kutekeleza haki ya wananchi wa kusini, tupate fursa kuhakikisha hizi mbinu ambazo walizifanya za diwani wetu kutusaliti tuwarudishie salamu watu wa CCM hatukubali kusalitiwa,” alisema Lipumba.

Aidha Lipumba ameweka wazi kwamba alimkubali Rais John Magufuli kwa mpango wake wa kupambana na rushwa, lakini kitendo cha CCM kurubuni madiwani nacho ni rushwa jambo ambalo hakubaliani nalo.

Upande wa chama cha CUF unaomuunga mkono, Prof. Lipumba unashiriki uchaguzi uliotangazwa na Tume ya Taifa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, huku upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu Maliim Seif ukiwa na msimamo wa kutoshiriki kwa madai ya kwamba kwa sasa wanashughulikia migogoro inayoendelea ndani ya chama.


from MPEKUZI

Comments