Joto la kisiasa likiwa limepamba moto kwa wanachama wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kukihama chama chao na kukimbilia CCM, Mwenyekiti Freeman Mbowe amesema hatishiki juu ya hilo bali anaona kama wanazidi kukiimarisha na kuwa na nguvu zaidi.
Kauli hiyo ya Mbowe imekuja kufuatia matukio ya Wabunge wa ndani ya CHADEMA pamoja na madiwani kujivua nyadhifa zao katika nyakati tofauti tofauti huku baadhi yao wakidai wanaelekea chama tawala (CCM) kwa lengo la kumuunga mkono Rais Magufuli katika utendaji wake wa kazi na wengine wakisema hawaridhishwi na utendaji wa chama hicho kwa madai kuna sera ya ubaguzi na kutokuwepo suala la uchaguzi la viongozi ndani ya chama hicho.
"Wale wanaokimbilia vyama vingine wanakiimarisha zaidi chama chetu kwa sababu kina tupa fursa ya kubaki na viongozi na wanachama wenye uchungu na nia ya dhati ya kukijenga chama chao. Wanaofika bei kwa ahadi ya fedha au vyeo waondoke mapema na nina wahakikishia CHADEMA itaendelea kuwa taasisi imara zaidi kuliko ilivyo sasa", amesema Mbowe.
Ndani ya siku tatu, Wabunge wawili wamejiuzulu kutoka CHADEMA wakielekea CCM ambapo jana Julai 30, 2018 aliyekuwa Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga alitangaza kurudi CCM alipokuwa awali, Julai 28, 2018 naye aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara alitangaza kukihama chama hicho.
Kalanga anakuwa Mbunge wa tatu CHADEMA, kujivua ubunge ambapo Mbunge wa kwanza alikuwa Dkt. Godwin Oloyce Mollel ambaye Disemba 14, 2017 alijivua ubunge wake kwa kile alichokieleza ni kuenda kuunga mkono kazi za Rais Magufuli.
Kwa kipindi cha takribani miaka mitatu tayari wabunge watano wameshajivua nyadhifa zao, ambapo dimba lilifunguliwa na Lazaro Nyalandu kutoka CCM kwenda CHADEMA, Maulid Mtulia CUF kuelekea CCM, Godwin Mollel CHADEMA kwenda CCM, Waitara kutoka CHADEMA kurudi CCM na sasa Julius Kalanga kutoka CHADEMA kurudi CCM.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment