Chadema yajibu mapigo, yadai Waitara ni Muongo

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimedai sababu kubwa ya kuondoka aliyekuwa Mbunge wa Ukonga na mwanachama wa chama hicho, Mwita Waitara ni kutokana na hofu ya kukosa Ubunge mwaka 2020 kutoka na safu yake ya viongozi kushindwa kupata nafasi.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano ya Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema ikiwa imepita siku moja tokea Mbunge huyo kutangaza hadharani kujivua uanachama wake na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku kudai sababu kubwa ya yeye kuchukua maamuzi hayo ni kutokana na ugomvi wake na Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe ndani ya chama.

Sababu nyingine za Mwita Waitara kuondoka CHADEMA amedai kwamba ndani ya chama hicho hakuna ruhusa ya Mbunge kusema lolote, hakuna uchaguzi wa haki bali kuna pachika pachika pamoja na Mbowe kutotaka kushauriwa.

"Anaposema hakuna uchaguzi ndani ya chama ni muongo, jimbo la Ukonga tulifanya uchaguzi kuanzia ngazi ya chini kabisa ya misingi, tukaenda matawi, kata na hatimaye Wilaya. Mwita alikuwa amepanga safu yake ya viongozi ambayo imeshindwa na kulalamika sana kwanini safu yake ilishindwa..

"Walishindwa kutokana na wapiga kura waliamua kuchagua viongozi wengine na hicho ndicho kilimfaya Mwita kuwa na hofu ya kukosa Ubunge katika chaguzi zijazo na amelalamika kwa maandishi", amesema Mrema.

Mbali na hilo, Mrema amemtaka Mwita Waitara kutoa sababu za msingi za kuondoka ndani ya chama hicho nasio kufanya siasa nyepesi za kuchafuana.

Mwita Waitara amekuwa Mbunge wa pili kutoka CHADEMA kujivua Ubunge, ambapo Mbunge wa kwanza alikuwa Dkt. Godwin Oloyce Mollel mnamo Disemba 14, 2017 alitangaza kujivua rasmi uanachama wa chama hicho na kujiunga na CCM kwa madai ya kuunga mkono utendaji ya Rais Magufuli.


from MPEKUZI

Comments