Agizo La Rais Magufuli Kuhusu Fedha Za Mashujaa Kutumika Kuboresha Miundombinu Ya Barabara Latekelezwa
Mnamo mwezi Juni, mwaka 2018, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alitoa taarifa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ameagiza) fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kumbukumbu ya siku ya Mashujaa kiasi cha Shilingi milioni 308, zitumike kuboresha miundombinu ya barabara jijini Dodoma.
Kufuatia agizo hilo, Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), walipata kiasi cha Shilingi milioni 288 kwa ajili kuweka taa 57 kwenye barabara ya Emmaus-African Dream na taa 42 kwenye barabara ya Kisasa. kiasi cha shilingi milioni 20 walipewa Wakala wa Barabara Dodoma (TANROADS), kwa ajili ya kuhamisha taa ya kuongoza magari kutoka njia panda ya Area D na kuwekwa kwenye makutano ya barabara ya Emmaus.
Tayari TARURA wameanza kutekeleza agizo hilo kwa kuweka taa kwenye barabara ya Kisasa na Emmaus-African Dream. Kwa upande wa TANROADS-Dodoma, zoezi la kuhamisha taa ya kuongoza magari limetekelezwa, ambapo wakandarasi watakabidhi kazi hizo rasmi mwezi Agosti mwaka huu.
Akiongea wakati wa ukaguzi wa kazi hiyo katika barabara ya Emmaus-African Dream Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Profesa Faustin Kamuzora alifafanua kuwa, kuwekwa kwa taa kwenye barabara hizo ni utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais aliyetaka miundombinu ya barabara jijini Dodoma kuboreshwa, hali inayoongeza usalama kwa watumiaji wa barabara hizo pamoja na kupandisha hadhi ya jiji na makazi ya maeneo husika.
“Taa hizi ni za kisasa na zitasaidia uhifadhi wa mazingira kwakuwa zinatumia mwanga wa jua, Serikali inajitahidi kuboresha miundo mbinu ikiwemo barabara hii, hivyo wananchi ambao barabara inapita katika makazi yao hawanabudi kuilinda miundombinu ya taa hizi. Fedha za walipakodi zimetumika hapa itasikitisha kuona miundo mbinu ya taa hizi kukuta imeharibiwa” amesisitiza Kamuzora.
Awali, akielezea shughuli zinazoendelea katika barabara ya Emmaus-African Dream, Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Dodoma, Mhandisi Lusako Kilembe alibainisha kuwa taa hizo ni za kisasa na zina uwezo wa kuhifadhi umeme hivyo zitasaidia kupunguza ghrama za uendeshaji na uhakika katika matumizi ya barabara hizo.
Kampuni ya Mionzi Jua Ltd ndiyo inayofanya kazi ya kuweka taa katika barabara za Kisasa na Emmaus-African Dream, ambapo jumla ya kiasi cha Shilingi milioni 287.1 zitatumika kukamilisha kazi hiyo.
IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILINO SERIKALINI
OFISI YA WAZIRI MKUU
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment