Wabunge Zitto Kabwe na Cecil Mwambe leo Alhamisi Juni 28, 2018 wamemuomba Spika Job Ndugai kuitaka Kamati ya Maadili, Kinga na Madaraka ya Bunge kumhoji na kumchukulia hatua Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Adelardus Kilangi kwa madai kuwa amekipotosha chombo hicho cha Dola.
Zitto ambaye ni mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo) na Mwambe (Ndanda-Chadema) wametoa kauli hiyo leo bungeni mjini Dodoma wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2018.
Wakati Mwambe akizungumza katika mjadala huo, Zitto alisimama na kumpa taarifa kutokana na kile alichokuwa akizungumza.
“Juzi wakati mawaziri wakijibu hoja mbalimbali za wabunge, AG alipewa nafasi ya kuchangia. Sina hakika kama ni makusudi au kuna mtu alimwagiza kuamua kulidanganya Bunge,” amesema Mwambe.
Alinukuu kidogo kile alichokisema AG Kilangi kwamba, “pamoja na marekebisho yatakayoletwa na Serikali, kwamba hukumu iliyotolewa na mahakama Desemba mwaka 2000, fedha zilizokuwa zinakatwa za Export levy zilikuwa ni mali ya umma.”
Mwambe alipingana na maelezo yaliyotolewa na AG siku mbili zilizopita kuwa fedha za ushuru wa mauzo ya korosho nje ni za umma na Serikali ndio yenye mamlaka ya kupanga matumizi yake, akisema kuwa fedha hizo ni za wakulima.
Katika maelezo yake siku hiyo, Dk Kilangi alisema fedha za ushuru wa mauzo ya korosho nje ni za umma zinazokusanywa na bodi ya zao hilo kwa niaba ya Serikali, kwamba msimamo huo umetokana na uamuzi katika kesi zilizofunguliwa na Mfuko wa Korosho katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa na haujawahi kupingwa.
Wakati Mwambe akieleza hayo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William OleNasha alisimama na kupingana na maelezo yake na kubainisha kuwa kilichozungumzwa na AG ni sahihi.
Maelezo hayo yalimnyanyua Zitto na kubainisha kuwa kilichoelezwa na AG kuhusu kesi hiyo si sahihi
“Mwanasheria Mkuu wa Serikali alilipotosha Bunge kwa kusoma kesi ambayo haikuwapo bungeni na ninatoa hoja mheshimiwa Spika iagize kamati ya maadili imhoji AG kwa kulipotosha Bunge, aadhibiwe katika hili.”
Mara baada Zitto kueleza hayo, Mwambe alimuunga mkono akitaka mwanasheria mkuu huyo wa Serikali achukuliwe hatua.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment