Waziri Mpango Asema Ataitembelea Mikoa ya Kusini....Hakuna Wa Kumzuia na Yupo Tayari Hata Kufa

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amesema atatembelea mikoa ya Lindi na Mtwara licha ya vitisho vilivyopo na yuko tayari kufa, na kamwe hawezi kuihujumu mikoa hiyo kiuchumi na hakuna anayeweza kumzuia kuitembelea katika kutekeleza majukumu yake.

Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo leo, Bungeni jijini Dodoma wakati akihitimisha hoja yake ya Bajeti ya Serikali aliyoiwasilisha Juni 14 mwaka huu, ambapo amesisitiza kuwa hakuna mtu wa kumzuia na iwapo kuna mwenye chuki binafsi anamwombea msamaha kwa Mungu..

“Kama yupo mtu ana chuki binafsi na Philip Mpango namwombea msahama kwa Mwenyezi Mungu, na niwatahadharishe wanaokula fedha za umma wanakula sumu,” amesema Dkt. Mpango.

Waziri Mpango Ameongeza, “Mimi Philip Mpango siwezi kamwe kuwahujumu wakulima wa mkoa wa Lindi na niwahakikishe watanzania kuwa Mtwara na Lindi nitakwenda iwe kutimiza wajibu wangu na ni uhuru wangu na hata ikibidi kufa katika kulitumia taifa” ameongeza Waziri Mpango.

Amesema amewatumikia Watanzania wote bila ubaguzi, amefundisha wanafunzi wote wakiwamo wanaotoka mikoa ya Kusini bila upendeleo na amewahi kuwa mshauri wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete na hakuwahi kuwa na upendeleo.

Tayari baadhi ya wabunge wametishia kufanya maandamano iwapo Serikali haitatoa asilimia 65 za ushuru wa mauzo ya korosho nje kwa ajili ya maendeleo ya zao hilo, huku wakipinga mabadiliko ya Sheria ya Korosho yanayokusudiwa kufanywa na Serikali ili ushuru huo upelekwe katika Mfuko Mkuu wa Hazina.


from MPEKUZI

Comments