WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kumewezesha kukamatwa kwa wafanyabiashara wakubwa waliokuwa wakitamba kwamba hawawezi kuguswa.
“Sasa hivi dawa zinakamatwa kwelikweli na wale wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya waliokuwa wakijiita vigogo na kutamba kuwa hawakamatwi na hata wakikamatwa wanaachiwa, wameanza kuikimbia nchi,” amesema.
Ameyasema hayo leo (Jumanne, Juni 26, 2018) wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria kwenye Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani yaliyofanyika uwanja wa Gangilonga, mkoani Iringa.
Waziri Mkuu amesema Serikali baada ya kuanzisha Mamlaka hiyo, iliiwezesha kwa kuipatia rasilimali fedha, watendaji na vitendea kazi na tayari mafanikio yameanza kuonekana.
Amesema kila mmoja anapaswa kuliona suala hilo la dawa za kulevya kama jambo hatari kwa mustakabali wa Taifa letu na akasisitiza kuwa watu wasioneane haya katika vita hiyo kwa kuwataja wahusika kwa sababu huuzwa katika mitaa yao na wauzaji wanawafahamu.
“Nawasihi viongozi wa siasa, dini pamoja na vyombo vya habari, tuendelee kukemea kwa nguvu zote matumizi na biashara ya dawa za kulevya,” amesema.
Waziri Mkuu amesema matumizi ya dawa za kulevya yapo zaidi kwenye miji mikubwa hasa ya Dar es Salaam, Arusha, Tanga na Mwanza, pia kasi ya kuenea kwa matumizi hayo kwenye miji midogo nayo ni kubwa hasa katika mikoa ya Iringa, Dodoma na Mbeya na Morogoro.
Wakati huohuo,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama amesema tatizo la dawa za kulevya limeiathiri duniia na watu wengi wameathirika na janga hilo ikiwemo jinsia na rika zote.
Amesemabiashara ya dawa za kulevya imesababisha madhara makubwa mbalimbali nchini yakiwemo ya kiafya, kijamii, kiuchumi, kimazingira, kisiasa na kiusalama. Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni“tujenge maisha yetu, jamii yetu na utu wetu bila dawa za kulevya”
“Zipo dalili kwamba, endapo biashara hii itaachwa iendelee, athari zaidi zitajitokeza ikiwemo kuingiliwa kwa misingi ya kiutawala na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kwa manufaa yao binafsi,” amesisitiza.
Awali, mmoja wa waathirika wa dawa hizo Bi. Reja Chawe ambaye alitumia dawa hizo kwa muda wa miaka 15 na alianza kutumia akiwa kidato cha pili, alisema alianza akiwa kidato cha pili baada ya kushawishiwa na rafiki yake wa kiume na alianza kwa kutumia bangi.
Bi Reja alisema kwa sasa ameacha ila anaumia sana akiona vijana wenzake wanaitumia dawa hizo kwa sababu yeye alipata matatizo makubwa wakati akitumia dawa hizo ikiwa ni pamoja na kufanya kazi ambazo ni za kujidhalilisha.
“Nilikuwa naitwa majina mabaya, nililala makaburini na nilifanya kazi ya kuchimba makaburi ya watoto wachanga na kuwazika. Mimi nilikuwa napitisha hata mwezi bila ya kuoga, pia nilikuwa naiba. Sikupenda, ila mkumbo tu, nawaomba vijana wenzangu waachane na dawa za kulevya,” amesema.
Muathirika mwingine, Bi. Christine Mponzi ambaye bado anatumia dawa ameiomba Serikali imsaidie ili aweze kuachana na dawa hizo ambazo alianza kutumia miaka 25 iliyopita na sasa anasikia maumivu ila anashindwa kuacha kutumia dawa hizo.
Alisema dawa hizo zimesababisha atengane na familia yake, ambapo watoto wake wawili nao wamemkataa kutokana na hali aliyokuwa nayo.” Dawa za kulevya ni hatari mimi nilikuwa mzuri na nilikuwa na mume wangu na watoto wamenikataa kwa sababu mama yao wananiona sina hadhi. Nilianza kufanya biashara kabla ya kutumia,”.
Tayari Serikali imesikia kilio chake, baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista kumkabidhi kwa muendeshaji wa nyumba za upataji nafuu (sober house) ili aanze kupatiwa matibabu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment