Waziri Mkuu: NHC Mna Jukumu La Kuwafikia Watu Wa Chini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lina jukumu kubwa la kuhakikisha sekta hiyo inakua na kuwafikia watu wa kipato cha chini.

Amesema ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli inahimiza uchumi wa viwanda, hivyo sekta ya nyumba ina mchango mkubwa sana katika kuchochea ukuaji wa viwanda.

Ameyasema hayo jana (Jumamosi, Juni 30,2018) wakati akizindua mradi wa Singidani Commecial Complex, mjini Singida. Jengo hilo la biashara na ofisi limejengwa na NHC kwa ajili ya kupangisha wafanyabiashara na taasisi mbalimbali.

Waziri Mkuu amesema sekta ya nyumba ni mtambuka kwa kuwa huchochea ukuaji wa uchumi, kutoa ajira na kukuza uwekezaji wa viwanda vya vifaa vya ujenzi kama saruji, mabati, nondo, marumaru na vinginevyo, ambavyo  vinafungua fursa kubwa ya ukuaji wa viwanda.

Hivyo, Waziri Mkuu amesema wadau mbalimbali wanapaswa kuitazama sekta ya nyumba kama sekta mtambuka katika kuleta maendeleo endelevu ya uchumi na jamii kwa ujumla.

“Napenda kutoa pongezi kwa Shirika la Nyumba la Taifa kwa kujenga jengo hili zuri na la kisasa kabisa hapa mjini Singida. Vilevile, jengo hili limeboresha na kupendezesha mandhari ya mji wa Singida kwa kiwango kikubwa kabisa,” amesema.

Waziri Mkuu amesema amefurahi kusikia jengo hilo limesanifiwa na ujenzi wake kusimamiwa na Watanzania wenyewe, wakandarasi washauri wakiwa ni NHC wenyewe na kwamba Watanzania zaidi ya 600 walipata ajira wakati wa ujenzi.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Bw. Felix Maagi alisema mradi wa jengo hilo la ofisi na biashara la Singidani lililogharimu sh. bilioni 3.4 ulianza Januari 26, 2015 na kukamilika Februari 17, 2018 na linatarajia kuliingizia shirika pango ya sh. milioni 420 kwa mwaka. Tayari asilimia 50 ya jengo hilo  limepangishwa.

Mkurugenzi huyo alisema mbali na mradi huo wa Singidani, pia shirika limeendelea kukua na kuimarika katika utendaji wake ambapo thamani ya mali zote imeongozeka kutoka sh. trilioni 1.7 mwaka 2011 mpaka kufikia sh. trilioni 4.8 mwaka 2018.

Bw. Maagi alisema mapato ya shirika yamekua kutoka sh. bilioni 40 kwa mwaka 2011 hadi kufikia sh. bilioni 154 mwaka 2018.” Pia shirika linalipa gawio la Serikali kila mwaka na gawio hilo limekua kutoka sh. milioni 250 mwaka 2011 hadi sh. bilioni 1.2 kwa mwaka 2018,”

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi, wabunge wa mkoa wa Singida, viongozi wa dini na maafisa wa Serikali.


from MPEKUZI

Comments