WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Tanzania na Mtandao wa Aga Khan (AKDN ) una lengo la kuleta maendeleo ya Taifa.
Ameyasema hayo jana usiku (Jumatatu, Juni 25, 2018) jijini Dodoma wakati akizungumza na viongozi na wananchi waliohudhuria hafla ya siku ya IMAMAT pamoja na kuhitimisha maadhimisho ya mtukufu Aga Khan kuwa kiongozi wa mtandao huo kwa miaka 60.
Waziri Mkuu alisema maadhimisho hayo yanaonesha kujitolea kwa hali ya juu na kwa moyo wa dhati ya maisha ya Mtukufu Aga Khan katika kuwahudumia na kuwalinda watu hususan wanyonge.
"Leo hii jamii zetu zinanufaika na juhudi hizi za kujitolea kwa hali ya juu alikokufanya Mtukufu Aga Khan kupitia utoaji wa misaada hasa katika kuboresha maeneo ya huduma muhimu kama elimu na afya,” alisema.
Alisema rafiki huyo mkubwa wa Tanzania amechangia kwa kiasi kikubwa kuinua jamii kiuchumi hususan kwa kupigania kuboreshwa kwa huduma za afya na elimu kupitia uwekezaji unaofanywa na Mtandao huo wa AKDN.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa maadhimisho hayo yanatoa somo muhimu kuhusu haja ya kujitolea, na kufanya juhudi za kutosha katika kila jambo sambamba na kuwahusisha watu wengine.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema lengo hilo halina budi kuongozwa na nia ya kuboresha maisha ya watu kwa namna yenye staha.
Awali, Mwakilishi Mkaazi wa Mtandao wa Aga Khan, Bw. Amin Kurji aliipongeza Serikali kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.
Alisema Mtandao wa AKDN umeenea katika mataifa 35 ambako wanatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kwa Tanzania wanatekeleza miradi tisa ikiwemo ya kilimo, afya, maendeleo ya jamii na elimu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment