Wabunge Watakiwa kuwasilisha taarifa za mali zao Kabla ya Tarehe 25 Mwezi Huu

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewataka wabunge wote kuwasilisha taarifa za mali wanazomiliki kabla ya Juni 25, 2018.

Taarifa ya hiyo ya Sekretarieti imetolewa bungeni leo Juni 19, 2018 na Naibu Spika Dk Tulia Ackson.

Dk Tulia amesema Sekretarieti ilitoa muda kwa wabunge kuwasilisha taarifa za umiliki wa mali zao kwa kuwa wabunge wengi hawakutekeleza agizo hilo.

“Sekretarieti iliwataka kuwasilisha nyaraka kabla ya Juni 25, 2018 zinazohusu fedha zilizoko benki au taasisi zingine za fedha, hisa, majengo, nyumba, madeni, mashine, viwanda, mitambo, magari na aina nyingine za usafiri, madeni na mikopo kwa mali zote zilipo nje,” amesema.

Amesema mwakilishi wa kamishnaa atafika ofisini kwa Katibu wa Bunge kuchukua taarifa.

Mbunge wa Misungwe, (CCM) Charles Kitwanga amesimama akitumia kanuni ya 68(7) kuhusu tangazo hilo akihoji kuhusu wabunge ambao hawajapata barua.

 “Kwa wale ambao tulikuwa hatujapata barua, vithibitisho vyetu viko nyumbani, Juni 25 ni karibu sana na Juni 26 tunatakiwa kuwapo bungeni kupitisha bajeti, haiwezi kutolewa nafasi zaidi ili kupeleka viambatanisho baadaye?”Alihoji

Akitoa majibu ya mwongozo huo, Dk Tulia amesema kuna  makundi mawili; wale wanaotakiwa kuwasilisha vielelezo vya mali zao wafanye hivyo na kwa kundi la pili ni ambao hawakuwa na taarifa.

“Tutaangalia jinsi ya kuwasiliana nao ili kuona vitawasilishwa lini mara baada ya kurudi majimboni kwenu.” Amesema


from MPEKUZI

Comments