TRC yahamasisha wafanyabiashara wanaokwenda Uganda kutumia reli

Shirika la Reli Tanzania (TRC) limewataka wafanyabiashara wanaosafirisha mizigo kwenda Uganda kutumia njia ya reli kwa kuwa ni salama na nafuu.

Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Uendeshaji wa TRC Focus Makoye amewahakikishia wafanyabiashara kuwa shirika hilo limejipanga vilivyo kutoa huduma hiyo ambayo ilisitishwa miaka 10 iliyopita.

Makoye ameyasema hayo jana  jioni ya Juni 28 ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuanza kusafirisha  mzigo wa  tani 2400 za mafuta mali ya Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) unaopelekwa nchini Uganda.

Amesema kuanza kwa safari hizo ni hatua mojawapo ya kulifufua shirika hilo hivyo wafanyabiashara wachangamkie fursa hiyo.

"Ni furaha kubwa sana kwetu tumeanza safari hii tukiwa tumejipanga kabisa na tunawahakikishia wafanyabiashara kuwa tuko vizuri,

"Wote tunafahamu usafiri wa reli ndio wa gharama nafuu na uhakika, hivyo basi tunawakaribisha watu wengi zaidi ambao wanafanya biashara kati ya Tanzania na Uganda watumie usafiri huu,"amesema

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha lojistiki cha WFP Mahamud Mabuyu amesema wamevutiwa kutumia njia ya reli baada ya kuhakikishiwa usalama wa mzigo.

Kwa mujibu wa Mabuyu usafirishaji kwa njia hiyo pia unasaidia kuokoa dola 40 kwa kila tani ambayo ingesafirishwa kwa kutumia magari.

"Mwaka jana tulishasafirisha tani 16000 kwenda Dodoma na Isaka, mzigo wetu ulifika salama haikupotea hata mfuko mmoja,"

"Hilo limetuvutia na baada ya hizi tani 2400 kuondoka ndani ya muda mfupi tutapeleka tena tani 15,000 hiyo ni kudhihirisha ni kiasi gani tunaridhishwa na TRC,” amesema


from MPEKUZI

Comments