Mahakama Yakaraa Ombi la Mmiliki wa Shule ya Scolastica

Mahakama ya Hakimu mkazi mjini Moshi imelikataa ombi la mmiliki wa Shule ya Scolastica, Edward Shayo anayekabiliwa na shtaka la mauaji ya mwanafunzi wa shule hiyo la kwenda kutibiwa.

Shayo pamoja na mwalimu wa shule hiyo, Labani Nabiswa na mlinzi wa shule hiyo, Hamis Chacha, wanatuhumiwa kumuua mwanafunzi wa kidato cha pili shuleni hapo, Humphrey Makundi (16).

Ombi hilo limewasilishwa leo Juni 27  na wakili Elikunda Kipoko anayemtetea mfanyabiashara huyo, aliyeomba Mahakama itoe kibali kwa mtuhumiwa huyo akatibiwe ingawa hakusema mteja wake anaumwa nini.

Hata hivyo, Hakimu Mkazi Jullieth Mawole amesema ingawa kutibiwa ni haki ya mtuhumiwa, mahakama hiyo haina uwezo wa kutoa kibali hicho kwa vile haina mamlaka kusikiliza kesi za mauaji.

“Mgonjwa ana haki ya msingi ya kupewa matibabu lakini Mahakama hii haiuhusiki kutoa kibali, hivyo Magereza ndiyo inayohusika kumpeleka mtuhumiwa wao hospitali,” alisema na kuongeza:-

“Mimi sina mamlaka ya kumruhusu mtuhumiwa kupelekwa hospitali hiyo ni kazi ya Mahakama Kuu,”

Hayo yalijitokeza baada ya upande wa Jamhuri katika kesi hiyo ukiwakilishwa na wakili wa Serikali, Agatha Pima, kuitaarifu Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika kwa asilimia 100.

Baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo, Hakimu Mawole aliiahirisha kesi hiyo hadi Juni 29 mwaka huu, wakati washtakiwa watakaposomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo vitakavyotumika dhidi yao.

Mwanafunzi huyo anadaiwa kuuawa Novemba mwaka jana na mwili wake kutupwa mita 300 kutoka shuleni hapo na ukazikwa bila kutambuliwa, hadi ulipofukuliwa kwa amri ya Mahakama.


from MPEKUZI

Comments