Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uruguay Luis Suarez, amesema kwa sasa yupo FIT, tofauti na alivyoanza michezo ya hatua ya makundi katika fainali za kombe la dunia, zinazoendelea nchini Urusi.
Suarez ameweka wazi utimamu wake wa mwili, akiwa katika mkutano na waandishi wa habari uliokua unazungumzia mpambano wa leo wa hatua ya 16, ambao utawakutanisha na mabingwa wa soka barani Ulaya Ureno.
Mshambuliaji huyo wa klabu ya Barcelona ya Hispania, amesema katika michezo ya hatua ya makundi hakuwa katika kiwango kizuri japo alibahatika kufunga bao walipocheza dhidi ya wenyeji Urusi, lakini kwa siku kadhaa alizofanya mazoezi kwa ajili ya mchezo wa hii leo, anajihisi yupo katika kiwango bora.
“Nipo vizuri tofauti na nilivyokua mwanzo, nimejaribu kufanya mazoezi kwa kiwango kikubwa na nimefanikiwa, ninajihisi tofauti na ilivyokua katika mchezo wa kwanza dhidi ya Misri na kisha Urusi.
“Binafsi nilikua najitafakari mara baada ya michezo niliyocheza, nilifahamu sikucheza vizuri, nilitumia majibu ya maswali niliyokua najiuliza kufanya mazoezi katika kiwango cha hali ya juu, hadi ninazungumza nanyi, ninaamini kesho (leo) nitacheza vizuri sana.
“Kwa upande wa timu, kiujumla tupo tayari kwa mpambano dhidi Ureno, tutahakikisha tunacheza kwa ushirikiano wakati wote, ili tufanikishe lengo la ushindi na kusonga mbele kwenye hatua ya robo fainali.”
Uruguay ilimaliza katika nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa kundi la kwanza lililokua na wenyeji Urusi, Misri na Saudi Arabia, kwa kufikisha alama 9.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment