Kivuko cha MV Mwanza Chafanyiwa Majaribio Kwa Mara ya Kwanza

Kivuko kipya cha MV Mwanza kimeingia majini leo kwa mara ya kwanza kwa ajili ya majaribio, baada ya ujenzi wake kukamilika.

 Kivuko hicho kitafanya safari kati ya Kigongo na Busisi na kinatarajiwa kubeba abiria zaidi ya 1,000 na magari madogo 36.

Pia, kitawasafirisha abiria wa mikoa ya Mwanza kuelekea Geita, Kagera, Kigoma na nchi za Rwanda, Burundi na Congo.

Akizungumza wakati wa kushusha kivuko hicho kwenye maji, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Vivuko wa Wakala wa Umeme na Ufundi (Temesa), Kokombe King’ombe amesema kivuko hicho kimetengezwa kisasa na kitakuwa na uwezo kwenda kwa kasi zaidi ikilinganishwa na vingine vitatu vilivyopo sasa.

Kivuko hicho kilianza kujengwa Juni 2016 na Kampuni ya Songoro Marine ya wazawa wa jijini Mwanza kwa gharama ya Sh8.9 bilioni.

“Kuwa na vivuko vingi katika kivuko cha Bususi ni tija kubwa, mbali na kuimarisha huduma lakini pia itatusaidia hata sisi kuvifanyia matengenezo bora vinapoharibika bila kuathiri shughuli za usafirishaji,” amesema King’ombe

Mkurugenzi Mtendaji wa Songoro Marine, Salehe Songoro amesema kivuko hicho kimekamilika kujengwa ila kitakuwa kwenye majaribio kwa kipindi cha wiki tatu.

“Kuanzia Julai mwaka huu ndipo kitaanza kufanya kazi ya kuvusha abiria kutoka Kingongo wilayani Misungwi kwenda Busisi wilayani Sengerema,”amesema.


from MPEKUZI

Comments