Chenge aitaka serikali kuangalia upya katazo la kusafirisha madini ghafi

Mwenyekiti wa Bunge Andrew Chenge ameiagiza Serikali kuangalia upya katazo la kusafirisha madini ghafi (cabon) kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kwa sababu halikuzingatia athari watakazozipata wawekezaji wa mitambo ya uchenjuaji.

Chenge amesema hayo bungeni leo Juni 14 baada ya kuombwa mwongozo na wabunge wawili Stanislaus Mabula(Nyamagana_CCM) na John Heche ( Tarime Vijini-Chadema).

Miongozo hiyo imekuja baada ya taarifa iliyotolewa na Waziri wa Madini Angela Kairuki  kuhusu utekelezaji wa agizo la Spika la kuzuia usafirishaji wa kaboni,  baada ya hivi karibuni kuombwa mwongozo na Heche kuhusu suala hilo.

Katika majibu yake Kairuki amesema katazo hilo linalenga kuzuia utoroshwaji wa madini, ukwepaji wa kodi, ada za ukaguzi na ushuru wa huduma.

Akifafanua hayo, Kairuki amesema siku tisa baada ya katazo hilo hilo Serikali mkoani Geita imetoa vibali vya uchenjuaji 40 tofauti na vibali saba walivyokuwa wakitoa kabla ya katazo hilo.

Hata hivyo baada ya maelezo hayo Heche aliomba mwongozo  na kusema katazo hilo limewaathiri kiuchumi wafanyabiashara wanaomiliki mitambo ya uchenjuaji.

"Wengine mheshimiwa mwenyekiti walikuwa na mikopo katika taasisi za fedha wamesitishiwa ghafla. Watawezaje kujenga mitambo haraka haraka? “Amesema.

Naye Mabula amesema watu wanataabika kutokana na katazo hilo na kushauri kuwa Serikali inaweza kuongeza udhibiti na ikapata mapato yake bila kuweka zuio.

"Mwaka  2014 Serikali iliruhusu gesi kusafirishwa kwasababu  ni raslimali ya Taifa... Hawa watu wanataabika. Tatizo ni uchenjuaji ama usimamizi? Usimamizi unaweza kuimarishwa na Serikali ikapata mapato yake," amesema Mabula

Baada ya miongozo hiyo Chenge amesema miongozo hiyo imetokana na wabunge kutoridhika na majibu ya Serikali.

“Unapopiga marufuku na kuanza ( utekelezaji) leo leo, unapaswa kuzingatia upande wa pili pawe na nafasi. Mwongozo wangu Serikali muangalie tena lengo ni mpate mapato halali lakini tusitoe mkanganyiko."amesema.


from MPEKUZI

Comments