Vijana Kunufaika na Mikakati ya Kuzalisha Ajira

Na: Frank Mvungi – MAELEZO, Dodoma.
Serikali imesema kuwa imeandaa mikakati ya muda mfupi na muda mrefu ili kuwawezesha vijana kujiajiri na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo kwa ujumla.

Akijibu swali la mbunge viti maalum Mhe. Catherine Nyakao Ruge wakati wa kipindi cha maswali na majibu jana Bungeni, Jijini Dodoma,  Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana na Ajira Mhe. Antony Mavunde amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuongeza fursa za wigo mpana wa nafasi za ajira kupitia sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uwekezaji katika uchumi wa viwanda na utekelezaji wa miradi mikubwa kama ilivyoanishwa katika Mpango wa Pili wa Maendeleo Nchini.

“Tunatekeleza program ya Taifa ya kukuza ujuzi inayowezesha nguvu kazi ya Taifa kuwa na ujuzi stahiki na kutoa fursa kwa vijana kuwa na sifa ya kuajirika na kujiajiri katika sekta mbalimbali ili kuchochea maendeleo,” alisema Mhe. Mavunde.

Mhe. Mavunde amesema, Serikali itaendelea kusimamia Vijana kujiunga katika makampuni pamoja na ushiriki na vikundi vya uzalishaji mali ili kupatiwa fursa ya mikopo yenye masharti nafuu kupitia mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kwa lengo la kuwaongezea mitaji ya kufanya shughuli za kiuchumi.

Akizungumzia ujenzi wa uchumi wa Viwanda kwa niaba ya Waziri wa  Viwanda Biashara na Uwekezaji, Mhe. Mavunde amesema kuwa Serikali inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kupitia TIC, EPZA, Balozi zetu nje ya nchi pamoja na Serikali ngazi za Wilaya na Mkoa.

Uhamasishaji huo unaenda sambamba na kutoa vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi kupitia sheria za uwekezaji  (EPZ na SEZ). Aidha, Serikali kupitia Taasisi za SIDO, NDC na EPZA inatoa ushauri wa namna ya kuanzishwa viwanda vidogo sana, vidogo na vya kati na kuvilea ili vikue.

Aliongeza kuwa Serikali inayo mipango na mikakati inayolenga kuhakikisha kuwepo kwa mazingira wezeshi ya biashra na uwekezaji nchini, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na amani na usalama wa  nchi, kuondoa vikwazo kupitia sera na sheria wezeshi, uwepo wa miundo mbinu wezeshi na saidizi pamoja na upatikanaji wa taarifa muhimu kuhusu fursa za uwekezaji.

Serikali ya Awamu ya Tano imewekeza katika kuhakikisha vijana wanapata ajira kupitia ujenzi wa uchumi wa viwanda  pamoja na program mbalimbali za uwezeshaji wananchi kiuchumi katika maeneo yote hapa nchini.


from MPEKUZI

Comments