Ukipoteza Passport utatozwa 500,000 hadi 700,000 kupata nyingine

Kamishna wa Uhamiaji, Uraia na Passport, Gerald Kihinga amesema Mtanzania atakayepoteza hati ya kielektroniki ya kusafiria inayopatikana kwa Shilingi 150,000 atalazimika kulipa Shilingi 500,000 kupata mpya.

Pia aliongeza kuwa iwapo ataipoteza tena hiyo aliyoipata kwa Tsh. 500,000 basi atalipa Tsh. 750,000 ili aweze kupata nyingine.

Ameyasema hayo jana katika uzinduzi wa utoaji wa hati hizo ambapo tayari hati 15,101 zimeshatolewa kwa Watanzania tangu kuanza kwa utoaji huo January mwaka huu.

Alisema zipo kesi nyingi za watu kupoteza hati zao za kusafiria na baadhi yake ni zile zinazotokea katika matukio yasiyohitaji uwapo wake.

“Utakuta mtu anakuja kuomba hati mpya, ukimuuliza mazingira (ilivyopotea) anasema alikuwa akielekea Kariakoo kutoka Buguruni, sasa huko Kariakoo hati hiyo unaenda nayo ya nini? Tuzitunze hati hizi kwa sababu ni nyaraka muhimu kwa nchi yetu,” alisema Kihinga.

Alifafanua kuwa hakuna haja ya kuzunguka na hati hiyo kila mahali isipokuwa yale maeneo muhimu yanayohitaji uwapo wake kuepuka gharama kubwa ya upatikanaji wake wakati inapopotea.

Pia, alieleza kuwa tangu kuanza kutolewa kwa hati hizo hakuna changamoto zilizojitokeza zaidi ya kuwapo baadhi ya watu wanaotumia mawakala kupata hati na hivyo kutozwa zaidi ya Sh300,000.


from MPEKUZI

Comments