Serikali Yatoa Bilioni 4 Kwa Watafiti Walioshinda Andiko la Miradi

Serikali  kupitia Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), imetoa Sh. bilioni 4.16 kwa ajili ya taasisi na watafiti walioshinda maandiko ya miradi ya utafiti yenye mchango wa uendelezaji na uimarishaji wa viwanda na kuifikia uchumi wa kati.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akikabidhi hundi ya kiasi hicho cha fedha kwa taasisi zilizoshindwa kupitia shindano lililoshindanisha zaidi ya maandiko 160.

Prof. Ndalichako alisema miradi hiyo iliyofadhiliwa imelenga kwenye nyanja za kusaidia kukuza viwanda vya dawa za binadamu na kuongeza ufanisi katika sekta ya mifugo kupitia uboreshaji wa mitambo na chanjo.

Alisema Costech ilishindanisha taasisi za utafiti na vyuo vikuu na kupata miradi nane ya uboreshaji wa miundombinu yenye thamani ya Sh. bilioni 3.2.

Pia alisema Costech kwa kushirikiana na Tume ya Mipango Zanzibar, ilishindanisha watafiti na kupokea maandiko ya miradi ya utafiti ikilenga kutafuta ufumbuzi wa matatizo maalumu ya visiwani humo.

“Maeneo ambayo yalilengwa ni utalii, endelevu, kilimo biashara, kilimo bahari na magonjwa yasiyoambukiza, miradi nane yenye thamani ya jumla ya Sh. milioni 960 ilipata ufadhili,” alisema.

Alisema jumla ya miradi yote iliyoshinda imepatiwa jumla ya Sh. bilioni 4.16.

Prof. Ndalichako aliwaasa watafiti na taasisi zilizopata fedha hizo za walipa kodi wazitumie kwa uadilifu na kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Fedha hizi ni za walipa kodi sio za sherehe bali kwa ajili ya kufanya utafiti, naomba zitumike kwa uadilifu mkubwa, serikali inadhamira ya kuimarisha viwanda na kuviendeleza vilivyopo, fanyeni utafiti ili tujue njia sahihi za kuimarisha uchumi wa viwanda,” alisema.

Mkurugenzi wa Costech, Dk. Amos Nungu, alisema jumla ya tungo 155 ziliwasilishwa mwezi Februari mwaka huu na baada ya mapitio, 86 zilikidhi vigezo na kupelekwa kwa wataalamu kwa mapitio na uchambuzi.

“Tungo 69 zilikosa sifa za awali na 41 zilishinda na kustahili ufadhili, lakini kwa sababu ya uhaba wa bajeti, miradi nane ilichaguliwa kwa kuzingatia mchango itakayotoa katika dira ya nchi ya uendelezaji wa viwanda,” alisema.

Mwenyekiti wa Costech, Prof. Makenya Maboko, alisema tume imejielekeza zaidi katika kufadhili miradi yenye tija na matokeo chanja yanayochangia moja kwa moja kwenye maendeleo ya Taifa ili kuinua maisha ya watu wengi.

Pia alisema tume imefadhili miundombinu ya utafiti wa udongo, uzalishaji wa mbegu bora za mimea hususan migomba na mizabibu na Imefadhili upanuzi wa maabara ya kuchakata mazao ya kilimo.



from MPEKUZI

Comments