Maoni ya mzee mshauri wa mahakama katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya bilionea Erasto Msuya, Herry Msangi jana yalimfanya dada wa marehemu, Antuja Msuya kuangua kilio mahakamani.
Wakitoa maoni yao mbele ya Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo, Msangi na mwenzake, Marry John waliiomba mahakama iwaone washtakiwa wote hawana hatia na iwaachie huru.
Hata hivyo wakati akiahirisha kesi hiyo, Jaji Maghimbi alisema amesikia maoni ya wazee hao na kwamba yatatiliwa maanani, lakini hayaifungi mahakama katika uamuzi wake.
Kabla ya kuahirisha kesi hiyo hadi hapo itakapotolewa notisi ya tarehe ya kusomwa kwa hukumu, Jaji Maghimbi aliwataka mawakili wa pande zote mbili kukutana naye kwa faragha katika chemba yake.
Mawakili hao ni wa Serikali, Tamari Mndeme na Ignasi Mwinuka na wale wa utetezi ambao ni Hudson Ndusyepo, Majura Magafu, Emmanuel Safari na John Lundu.
Msangi ndiye aliyekuwa wa kwanza kutoa maoni yake kwa muda wa saa 1:40 kuanzia saa 4:30 asubuhi hadi saa 6:10 mchana na kufuatiwa na Marry aliyetoa kwa dakika tano kuanzia saa 6:20 mchana.
Mara tu alipomaliza kutoa maoni yake hayo, dada wa marehemu alianza kuangua kilio kwa sauti ya juu huku akitoka kortini, na alipotoka hatua tatu kutoka mlangoni aliongeza sauti.
“Nimeshindwa kuvumilia. Nifungeni. Nasema nifungeni,” alisikika akisema huku akiendelea kulia kabla ya polisi waliokuwepo kumuondoa na kumpeleka mbali.
Akitoa maoni yake, Msangi alisema yangejikita katika mambo matano ambayo ni simu iliyotuma meseji kwa marehemu na usajili wake na pikipiki mbili zinazodaiwa kutumika katika mauaji.
Pia alitaja mambo mengine aliyodai anayaeleza bila kigugumizi kuwa ni SMG inayodaiwa ilitumika katika mauaji, kifaa cha DVR ya kamera ya CCTV na maelezo ya kukiri kosa ya washtakiwa wanne.
Msuya aliyekuwa akimiliki vitega uchumi kadhaa ndani na nje ya Arusha, aliuawa kwa kutumia bunduki ya kivita ya SMG, Agosti 7, 2013 katika eneo la Mijohoroni wilayani Hai.
Msangi alidai ushahidi wa mashtaka unadai simu namba 0682405323 ilituma meseji kwa marehemu Msuya tarehe 6.8.2013 ukisema, “nina riziki” na tarehe 7.8.2013 ikatuma mwingine, “nipo Kia nakusubiri”.
“Tofauti na maneno ya mdomoni (ya mashahidi) meseji hiyo sikuiona hapa mahakamani ikionyeshwa. Pamoja na kutoonyeshwa tuliambiwa laini ilisajiliwa kimakosa kwa jina la Motii Mongululu,” alidai.
Akitoa maoni yake, Msangi alidai mashahidi hao wa upande wa mashtaka walidai aliyekwenda kusajili laini hiyo ni mtu anayeitwa Adam Leani na ilikuwa ikitumiwa na mshtakiwa wa saba, Ally Mjeshi.
“Hakuna ushahidi wowote ulioletwa kuonyesha Mjeshi aliwahi kutumia jina la Motii Mongululu wala hakuna ushahidi kuwa alifika eneo la kusajilia simu na kujitambulisha ni Adam Leani,”alieleza.
“Mahakama ione laini ile ilisajiliwa kihalali kwa sababu kama ilikuwa kweli imesajiliwa kimakosa, hakuna mtu aliyewajibishwa kwa usajili huo. Hiyo laini ni halali kwa mtu anaitwa Motii Mongululu”.
“Ushahidi huo usihusishwe na Ally Mussa Mjeshi wala usimhusishe mshtakiwa mwingine yeyote aliyepo kizimbani. Ibaki kuwa mali halali ya Mongululu ambaye sio mshtakiwa hapa mahakamani”.
Pikipiki mbili zilizowabeba wauaji
Kuhusu pikipiki mbili King Lion namba T751 CKB na Toyo namba T316 CLG ambazo mashahidi wa upande wa mashtaka walizihusisha na washtakiwa, Msangi alitaka wasihusishwe nazo.
“Hakuna hata pikipiki moja iliyokamatwa ikiwa na mshtakiwa na hakuna ushahidi kuwa ilikamatwa katika eneo linalomilikiwa na mshtakiwa wala hakuna ushahidi yuko aliyewahi kuzimiliki,” alieleza.
“Muuzaji wa pikipiki aliyekuja hapa mahakamani (Flotea Mmasy-shahidi wa 20) hakuweza kumtambua mshtakiwa yeyote kuwa ndiye aliyemuuzia pikipiki hizo.
“Kwa ushahidi huo ni vigumu kumhusisha mshtakiwa yeyote na vidhibiti hivyo vya mahakama. Niombe pikipiki hizo zisihusishwe na Sadik Jabir (mshtakiwa wa sita) wala mshtakiwa mwingine.”
SMG iliyotumika kwenye mauaji
Kuhusu bunduki aina ya SMG yenye namba 1952 r KJ 10520, inayodaiwa ilinunuliwa na mshtakiwa wa kwanza, Sharifu Mohamed, mzee huyo wa mahakama alisema kielelezo hicho kina utata.
“Inaonyesha iliokotwa mara tatu siku tofauti. Kwanza iliokotwa na shahidi wa 11, SP Vicent Lyimo Septemba 11,2013 na ikaokotwa Septemba 13,2013 na shahidi wa tisa, Inspekta Samwel Maimu,” alisema Msangi.
Alisema bunduki hiyohiyo iliokotwa na shahidi wa 27, Inspekta Damian Chilumba Septemba 14,2013 na wote wanadai waliipata kwenye Tindiga Sanyajuu.
“Mashahidi hao ni maofisa wa polisi wenye vyeo vikubwa. Silaha ni hiihii moja iliyoletwa mahakamani na kila mmoja aliitambua hapa mahakamani ni hiyo. Hilo linaacha maswali,” alidai.
“Kwa nini bunduki hiyo hiyo ipatikane siku tofauti tofauti? Hakuna mahali hao mashahidi waliieleza mahakama kuwa walisahau. Hakuna mshtakiwa yeyote alikamatwa nayo. Udhaifu huo ni mkubwa.
“Hakuna ushahidi wa finger print (alama za vidole) ulioletwa kuthibitisha ni nani alishika bunduki hiyo na kumfyatulia risasi marehemu. Isihusishwe kabisa na Karim Kihundwa (mshtakiwa wa tano).”
Akitoa maoni yake kuhusu kifaa cha kuhifadhi kumbukumbu (DvR) cha kamera za usalama (CCTV), iliyochukuliwa na polisi kutoka kwa Sharifu, Msangi alihoji matokeo ya uchunguzi wake.
“Tunaelezwa na mashahidi kuwa washtakiwa walikula njama na pikipiki mbili zilizonunuliwa zilihifadhiwa nyumbani kwa Sharifu na kuna CCTV camera na DvR ilichukuliwa na polisi,” alidai.
Msangi alidai kama ni kweli pikipiki hizo zilipelekwa kwa Sharifu, uchunguzi katika kifaa hicho ungeonyesha zikiingizwa ndani ya nyumba hiyo lakini hakuna ushahidi kuwa waliona nini.
“Ushahidi wa kwamba pikipiki zilizotumika katika haya mauaji zilipelekwa nyumbani kwa Sharifu usizingatiwe na wala Sharifu asihusishwe nao,” alieleza mzee huyo.
Pia alihoji ilikuwaje hakuna shahidi hata mmoja kutoka nyumba ya kulala wageni ya Shamoo inayomilikiwa na Sharifu inayodaiwa ilitumika kupanga njama aliyeitwa kutoa ushahidi.
Maelezo ya kukiri ya washtakiwa
Mzee huyo alieleza katika maoni yake kuwa anavyoona maelezo ya washtakiwa wanne; Sharifu, Mussa Mangu, Karim Kihundwa na Ally Majeshi yalitolewa kwa kuteswa.
“Naomba niamini waliteswa kwa sababu Mjeshi alitoa maelezo kwa mlinzi wa amani akiwa huru, lakini hayakuletwa na badala yake wakaleta yale ya onyo ya polisi anayoyalalamikia alilazimishwa,” alieleza.
Akitolea mfano wa maelezo ya Sharifu, Msangi alidai aliwataja Joseph Mwakipesile au Chussa na mtu mwingine, lakini watu hao si miongoni mwa washtakiwa wa kesi hiyo ya mauaji.
“Kama hayo maelezo yalionekana ni ya uongo ndio maana Chusa na mwenzake wakaachiwa, basi mahakama iyaone maelezo hayo ni ya uongo na imuachie mshtakiwa wa kwanza (Sharifu),” alisema.
“Kwa mazingira hayo ya ushahidi ulioletwa hapa mahakamani ni maoni yangu una madhaifu makubwa kwa washtakiwa na washtakiwa walilazimishwa kusaini maelezo baada ya kuteswa.”
Kwa upande wake, mzee wa mahakama Marry John alizungumza kwa muda usiozidi dakika tano akisema anaunga mkono yote aliyoyasema mzee mwenzake isipokuwa akaongeza mambo machache.
“Inaonekana washtakiwa waliteswa sana ndio maana wakasaini hayo maelezo ya kukiri kosa. Zile tarehe za mashahidi (kupatikana bunduki na kukamatwa kwa washtakiwa) zilikuwa tofauti tofauti,” alisema.
“Washtakiwa siku ya mauaji hawakuwepo na wengine walikuwa harusini. Mahakama iwaone washtakiwa wote hawana hatia na waachiliwe huru.”
Awali Jaji Maghimbi aliwakumbusha wajibu wao kuwa ili kuthibitisha shtaka la mauaji ni lazima ithibitike kuwa kuna kitendo kilifanyika au kiliachwa kufanyika na kusababisha kifo.
Pia aliwaambia ni lazima pawepo na nia ovu na mshtakiwa alikuwa anajua kifo hicho ni matokeo ya kitendo alichofanya na pia ushahidi wa mazingira unaegemea ushahidi wa vipande vipande.
Jaji aliwaeleza ni lazima kuwepo na njama ya kutenda kosa hilo na kwamba kupokewa kwa maelezo ya kukiri kosa, sio lazima yazingatiwe moja kwa moja kwani ni lazima pawepo ushahidi huru unaounganika.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa Agosti 5, 2010 na hadi inafikia mwisho ili kusubiri kupangwa kwa tarehe ya hukumu, upande wa mashtaka uliegemea ushahidi wa mashahidi 32 wakati utetezi mashahidi wanane.
Chanzo: Mwananchi
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment