Serikali yabeba jukumu la kumtibu Mzee Majuto

Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amemtembelea msanii nguli wa filamu, Amri Athuman maarufu mzee Majuto na kueleza kuwa Serikali inabeba jukumu la matibabu yake.

Mzee Majuto alilazwa Aprili 23 baada ya kuzidiwa ghafla kutokana na kidonda cha operesheni ya henia aliyofanyiwa Julai mwaka jana jijini Tanga.

Akizungumza katika tukio hilo jana Aprili 28, 2018 Dk Mwakyembe amesema Serikali imeamua kumpeleka mzee Majuto nchini India kwa ajili ya matibabu zaidi.

 "Kwa kuanzia, tumeamua kumhamishia mzee Majuto katika hospitali ya Muhimbili ili kukamilisha maandalizi muhimu kabla ya safari ya India," amesema Dk Mwakyembe.

Amesema matibabu atakayopata mzee Majuto akiwa Muhimbili na akiwa nchini India yatagharamiwa na Serikali.

Katika hatua nyingine, kampuni zilizowahi kufanya kazi na mzee Majuto zimeitikia wito wa kumchangia huku Dk Mwakyembe akitoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kumchangia ili kuwezesha familia yake kujikimu katika kipindi hiki ambacho anapatiwa matibabu.


from MPEKUZI

Comments