Serikali kuendelea kukomesha ajira hatarishi za watoto

Serikali imedhamiria kuendelea kukomesha ajira hatarishi za watoto ili kuhakikisha kuwa watoto wanalindwa na kuwapa nafasi stahiki kulingana na sheria na kanuni zilizopo nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama alipohudhuria katika kilele cha Siku ya Afya na Usalama Mahali Pa Kazi Duniani inayoadhimishwa kila mwaka Aprili ambapo Kitaifa ilifanyika Mkoani Iringa.

Amesema kuwa katika mapambano hayo ya ajira hatarishi kwa watoto ni moja ya utekelezaji wa kampeni zinazolenga kuharakisha utekeleezaji wa vipaumbele vilivyomo kwenye lengo namba (8) la maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ambalo ni kuboresha mazingira ya wafanyakazi na kukomesha ajira mbaya kwa watoto.

“Tuendelee kupiga vita ajira mbaya kwa watoto kwa kuzingatia kampeni zilizopo hasa ile ya kuboresha mazingira ya wafanyakazi ifikapo mwaka 2030 pamoja na kukomesha ajira mbaya za watoto ifikapo mwaka 2025,” amesema Mhagama

Aidha, amesema kuwa katika kuhakikisha watoto wanakuwa na mazingira salama, lazima kuwe na mikakati  ya pamoja baina ya utatu katika masuala ya kazi na ajira ikiwemo na kujenga utamaduni wa kujikinga na vihatarishi sehemu za kazi vinavyoweza kusababisha kuhatarisha afya na usalama wa wafanyakazi.

Aidha kama Taifa lazima tuoneshe umuhimu wa kuhakikisha kampeni hii inakuwa na matokeo chanya na kuendelea kuwa na Taifa lenye maendeleo.

Hata hivyo, ameongeza kuwa kulingana na matokeo ya Utafiti wa Mtakwimu Mkuu wa Serikali uliofanyika mwaka 2014 na matokeo yake kuchapishwa mwaka 2016 ulibainisha kuwa, hali ya ajira  hatarishi za watoto kuzidi kuwa mbaya zaidi katika sehemu za mashambani, sekta ya madini, misitu na uvuvi.


from MPEKUZI

Comments