Rais Magufuli amlilia Abbas Kandoro

Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi za kifo cha mkuu wa mkoa mstaafu, Abbas Kandoro akisema Taifa limepoteza mtu muhimu ambaye mchango wake hautasahaulika.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa aliyoitoa leo Aprili 28, 2018 amesema Rais Magufuli Kandoro alikuwa kiongozi shupavu, aliyejiamini na kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na taratibu, aliwapenda watu aliowaongoza na alidhirisha uzalendo wa kweli.

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mkuu wa Mkoa mstaafu Abbas Kandoro, nawapa pole wana familia, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na msiba huu,” amesema Rais Magufuli na kuongeza:

“Tumempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake katika utumishi kwa umma katika nyadhifa mbalimbali zikiwemo mkuu wa mkoa, mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri hautasahaulika.”

Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza kufikisha salamu hizo kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo.

“Nimesikitishwa sana na kifo chake, nawaombea wafiwa wote wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahilivu katika kipindi hiki cha majonzi na pia namuombea marehemu Abbas Kandoro apumzike mahali pema peponi, Amina,” amesema Rais Magufuli

Enzi za utumishi wake, Kandoro amehudumu mikoa ya Tabora, Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya.

Kandoro alifariki jana Aprili 27, 2018 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na anatarajiwa kuzikwa kesho Aprili 29, 2018 mkoani Iringa.


from MPEKUZI

Comments