JUMLA ya akinamama 20,815 waliofanyiwa uchunguzi wa saratani ya mlango wa shingo ya kizazi mkoani Pwani katika kipindi cha miaka mitatu kati yao 530 walikutwa na dalili za awali za saratani hiyo,ambapo watatu walifariki.
Aidha kati ya akinamama hao waliofanyiwa uchunguzi akinamama 412 walitibiwa matibabu na 115 walipata rufaa ya kwenda Oceanroad na hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.
Akitoa takwimu hizo ,wakati wa uzinduzi wa zoezi la chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa shingo ya kizazi kwa watoto wenye umri wa miaka 14 ,kimkoa yaliyofanyika kituo cha afya mkoani,Kibaha,mganga mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Yudas Ndungile alisema , ipo changamoto ya kutojua idadi ya vifo kamili kwa kuwa wengi hupata rufaa.
Pamoja na hayo ,alisema ipo haja ya kuona ukubwa wa tatizo hilo kwa kuangalia afya mapema na watoto wa mashuleni kupata chanjo.
Ndungile alisema jumla ya watoto wa kike 18,823 waliopo shule na nje ya shule mkoani hapo watapatiwa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi mwaka huu.
Alielezea, tayari wameshapokea chanjo na wataanza kuzitoa katika vituo mbalimbali vya huduma.
Ndungile aliitoa shaka jamii kuwa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi ni salama ,haina madhara na haiathiri uwezo wa binti kupata watoto hapo baadae
” Serikali imethibitisha usalama wa umadhubuti wa chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi ndiyo maana imeiongeza kwenye mpango wa Taifa wa chanjo ili iweze kusaidia kudhibiti tatizo hilo kwa akinamama”:
Ndungile alieleza mwaka 2018 chanjo itatolewa kwa wasichana waliofikisha umri wa miaka 14 na ili kupata kinga kamili walengwa watahitaji kupatiwa dozi mbili.
Alisisitiza chanjo hiyo huwakinga wasichana wasipate saratani ya mlango wa kizazi pindi wawapo watu wazima wakiwa na familia zao.
“Nchini Tanzania saratani ya mlango wa kizazi ni ya kwanza kwa vifo ikifuatiwa na saratani ya matiti ” Saratani hizi mbili kwa pamoja husababisha zaidi ya asilimia 50 ya vifo vyote vya wakinamama vitokanavyo na saratani”alibainisha Ndungile.
Kwa upande wake ,Mganga mkuu wa halmashauri ya Mji wa Kibaha ,Dkt.Tulitweni Mwinuka alisema ,wamezindua chanjo hiyo kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.
Alielezea ,kiwilaya wamezindua chanjo hiyo kwa wasichana 100 kituoni hapo na wanatarajia kufanikisha na kuleta matokeo kutokana na chanjo hiyo .
Akizindua zoezi hilo ,kwa niaba ya mkuu wa Mkoa wa Pwani,mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama aliwataka wanafunzi wa kike kuacha kujiiingiza kwenye vitendo vya ngono mapema ili kujiepusha kuingia kwenye hatari ya kupata magonjwa ya zinaa,ukimwi na hata saratani ya mlango wa kizazi.
Alisema moja ya sababu zinazosababisha saratani hiyo ni kuwa na wanaume wengi ,kuvuta sigara ,wenye mitala, na kuanza mapema kufanya ngono.
“Acheni kujiingiza kwenye mapenzi mapema ni hatari katika maisha yenu, ukivua sketi ,na mwanaume akavua suruali jua kuna hatari ya kuhatarisha maisha yako kwa magonjwa yanayosababishwa kutokana na ngono”
“Jizuieni hadi hapo mtakapoolewa ,msikimbilie ngono za haraka,mtapata saratani”: alisisitiza Mshama.
Mshama aliwahimiza wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao wa kike wenye umri wa miaka 14 kupata chanjo hiyo kwani haina madhara.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment