Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Jijini Dar es salaam, Lazaro Mambosasa, ametolea ufafanuzi suala ambalo limeanza kushika hatamu mitandaoni la kukamatwa kwa Katibu wa Baraza la Wanawake CHADEMA kata ya Kisutu Elizabeth Mambosho na kupelekwa rumande akiwa na mtoto mchanga.
Kamanda Mambosasa amesema mwanamke huyo alishaachiwa kwa dhamana, na kwamba kesi yake inachunguzwa na makao makuu, licha ya kutoweka wazi sababu ya kukamatwa kwake.
“Alikamatwa wakati mimi nipo safarini na alishadhaminiwa, na kesi yake inapelelezwa makao makuu, lakini sijui sababu ya kukamatwa kwake labda muwaulize makao makuu”, amesema Kamanda Mambosasa.
Taarifa za kukamatwa kwa Elizabeth zimezagaa mitandaoni huku watu wakilalamikia kitendo cha kukamatwa akiwa na mtoto wake mchanga aliyejifungua wiki tatu zilizopita, huku akiwa na mshono kwani imeelezwa alijifungua kwa njia ya upasuaji.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment