Majonzi Yatawala, Kuagwa Kwa Mwili Wa Mtoto Aliyechomwa Kisu Na Dada Yake

Mtotro Joshua Michael (2) aliyeuawa na dada yake Delta Kalambo (19) kwa kuchomwa kisu kwenye kitovu na mwili wake kufichwa uvunguni unazikwa leo Sengerema mkoani Mwanza.

Simanzi ilitawala watu waliojitokeza kuuaga mwili wa mtoto huyo nyumbani kwao Kigamboni jana huku baadhi wakieleza kuumizwa na unyama uliofanyika kwa mtoto huyo.

Tukio la kuuliwa kwa mtoto huyo lilitokea Jumatatu katika eneo la Tungi Mwembepoa, Kigamboni jijini Dar es Salaam wakati mama wa mtoto ambaye ni muuguzi wa Hospitali ya Mkuranga, Magreth Kasedi, akiwa kazini.

Msemaji wa familia ambaye ni baba mkubwa wa marehemu, Deus Philipo, jana alisema marehemu huyo atazikwa leo mkoani Mwanza.

Alisema mazishi yatafanyika katika kijiji cha Nyabila endapo wasingekutana na changamoto barabarani.

"Nashindwa kusema tutazika kesho (leo) kwa sababu hatujui huko njiani safari itakuwaje ila tukifika mapema tutazika," alisema.

Kasedi alisema  juzi kuwa Jumatatu aliamka asubuhi kama kawaida na kumuacha mtoto wake na Delta ambaye ni mtoto wa dada yake.

Alisema aliporudi alishangaa kukuta mwanawe wala Delta hawapo nyumbani na ndipo "Nikaingaika kumtafuta mtoto... kila sehemu".

"Kwa majirani... hayupo. Nikahangaika kupiga simu yake haipatikani, lakini wakati nipo kazini nilipata ujumbe mfupi kutoka kwa Delta kuwa nimpigie mtu fulani lakini ujumbe huo sikuuelewa anamaanisha nini."

Alisema kuwa alimpeleka Delta kwenye mafunzo ya ufundi cherehani hivyo alipoona msichana huyo na mtoto hawaonekani nyumbani aliamua kumpigia simu fundi mwalimu wake kujua kama amemuachia mtoto wake.

"Nilimuuliza kama kaachiwa mtoto wangu akaniambia Delta kaja majira ya saa tatu asubuhi bila mtoto," alisema na kueleza zaidi:

"Lakini nilipofika nyumbani kuingia ndani nikakuta ndoo ya bafuni iko sebleni ikiwa na brashi ndani. Nikaenda mezani nikakuta ujumbe mrefu sana.

"Sehemu ya ujumbe huo ulisema mama naomba unisamehe mimi nimekuwa mkaidi, umenionya mara nyingi sana kwa hiyo naomba unisamehe... naenda nyumbani.

"Yaani kaandika mengi nikashindwa kuendelea, nikaamua kutoka nje kumtafuta mtoto kwa majirani kwa kudhani kuwa huenda atakuwa kamuacha kwasababu kaandika anataka kwenda kwao."

Kasedi alisema alihangaika kwa majirani lakini hakuweza kumpata mtoto na ndipo waliposhauriana na majirani waende kutoa taarifa kituo polisi.

Alisema baada ya kutoka polisi walikwenda Stendi ya Steven, eneo la Kisiwani kwa ajili ya kumtafuta kijana anayejulikana kwa jina la Chasii Manyanya ambaye ana mahusiano ya kimapenzi na msichana huyo.

"Huyu kijana alikuwa akipigiwa simu anapokea na kuiacha hewani, ndipo tulipoenda kuhangaika kumtafuta hadi tukafanikiwa kuonyeshwa nyumba anayoishi," alisema mama huyo katika mazungumzo.

"Nilikaa hapo mpaka saa 4:45 usiku ndipo alipokuja huyo kijana, nikamuambia mimi ninachotaka ni mtoto wangu, sina haja na huyo msichana. Akaniambia mama sijaletewa mtoto."

Aliendelea kusimulia kuwa baada ya kuona hivyo alilazimika kutoa taarifa polisi na kijana huyo kushikiliwa huku wakifanya jitihada mbalimbali za kumtafuta Delta ili aeleze mtoto alipo.

Alisema ilipofika asubuhi ya Jumanne aliwahi kituo cha polisi wakasema wanamuangalia kwenye mitandao wajue alipo na ilivyofika saa nne aliiwasha simu ikiwa inaonyesha yupo eneo la Mikadi, Kigamboni.

"Kumbe mimi nahangaika kutafuta mtoto kumbe yuko chini ya uvungu wangu wa kitanda, yaani hakuna damu iliyomwagika," alisema mzazi huyo. "Baada ya kumchoma kisu kwenye kitovu akamlaza kifudifudi na kumfunika vizuri (uvunguni)."

Aidha, alisema mtuhumiwa huyo baada ya kuwasha simu yake majira ya nne aliwasiliana na fundi cherehani ambapo alipomuuliza alipo mtoto alimjibu kuwa amemuacha chumbani.

"Fundi aliwasiliana naye akamuelekeza alipo na kumuambia hataki mtu ajue ndipo fundi akachukua bodaboda kumfuata ili amuelekeze sehemu mtoto alipo," alisema.

"Na mimi nikamtumia ujumbe kwenye simu nikamuambia Delta sijawahi kukufanyia ubaya wowote katika maisha yako, naomba uniambie mtoto wangu alipo.

"Akanijubu kuwa Joshua yupo uvunguni."

Alisema alipopata huo ujumbe alimjulisha baba wa mtoto ausome kwa kuwa yeye alikuwa ameshindwa kuuelewa na ndipo walipofuatilia na kukuta mtoto yuko uvunguni mwa kitanda.

"Polisi walikuja na kuuchukua mwili wa mtoto lakini niliomba nimuangalie nijue... ndipo nikaona kamchoma na kisu kwenye kitovu na utumbo ulikuwa unatoka," alisema Kasedi.

"Hakuna jirani ambaye alisikia kelele za kulia kwa huyo mtoto, nasikia alifungulia mziki sauti kubwa."

Aliendelea kusimulia kuwa Delta alikamatwa baada ya mpenzi wake kuambiwa ampigie simu wakutane kwa ajili ya kumtafutia sehemu ya kuishi, kwasababu ametoroka nyumbani.

"Basi akamjibu yule kijana yuko tayari akamuelekeza alipo na ndipo polisi walipoongozana naye na kumkamata na kwa sasa yuko polisi."

Aidha, alisema hakuweza kuamini kama mtoto huyo ambaye alikuwa akimchukulia kama wake wa kwanza angeweza kufanya tukio hilo.

Alisema hakuwahi kugombana naye na kikubwa alikuwa akimuonya kitendo cha kumuingiza mpenzi wake ndani kwake kwani ni ukosefu wa maadili.

"Huyo mwanaume wake nimemfumania ndani kwangu mara mbili, nikamuonya maana huyu ni kama mwanangu... mtoto wa dada yako hana tofauti na mtoto wako."

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula, alithibitisha kutokea kwa tukio na kueleza kuwa wanamshikilia msichana huyo kwa ajili ya mahojiano ili sheria ichukue mkondo wake.

"Huyu msichana baada ya kufanya huu unyama aliuweka mwili chini ya uvungu wa kitanda na kwenda kujificha na tulipofanikiwa kumkamata tulimuambia atuonyeshe alipo mtoto akasema yuko chini ya uvungu wa kitanda wanapolala wazazi wa mtoto," alisema Kamanda Lukula.



from MPEKUZI

Comments