Kauli ya Balozi Dkt Slaa kuhusu Watanzania walioandamana nchini Sweden

Wakati polisi wakitoa tahadhari kwa wananchi kuhusu maandamano yaliyoratibiwa kwenye mitandao ya kijamii na kupangwa kufanyika leo, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbrod Slaa amesema ofisi yake ilipokea barua kutoka polisi wa nchi hiyo kuhusu taarifa za Watanzania waliotaka kuandamana jana.

Hata hivyo, hapa nchini polisi imeonya ikisema maandamano hayo ni batili na atakayeshiriki atashughulikiwa.

Akizungumza na gazeti la Mwananchi kutoka nchini Sweden, Dk Slaa alisema jana kuwa, polisi walisema wameshawapa kibali waandamanaji na watawapa ulinzi unaostahili.

“Ilipofika saa tatu asubuhi, walifika watu kumi, polisi hawakuwa na kazi kubwa waliwapangia wapi wasimame, walikuja na mabango yao. Lakini hakukuwa na muziki kwa sababu huku hawatakiwi kupiga muziki,” alisema.

Alisema baada ya kuwaona waandamanaji hao wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali, walikubaliana na polisi kuwa waingie ndani ili kujua nini wanachohitaji.

“Walikataa kuingia ndani na kusema hawana sababu ya kujadiliana. Tukawaambia tunawaomba watu viongozi wawili ili wawe wawakilishi na viongozi hao waseme nini wanachotaka, lakini pia walikataa,” alisema.

Dk Slaa alisema Sweden ni moja ya nchi zenye vyama vya Watanzania vilivyosajiliwa kuanzia ngazi ya mkoa na kuendelea na viongozi wa vyama hivyo walipiga simu ubalozini wakimsifu Rais Magufuli.

“Nimepokea simu kutoka sehemu mbalimbali, kwamba wanamuunga mkono Rais John Magufuli. Wanataka Rais asilegeze kamba katika vita dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya mali za umma kwa sababu vita hivyo vinatengeneza maadui ndiyo maana mambo kama haya
yanatokea,” alisema.

Kuhusu ujumbe aliosema ni wa upotoshaji ulioandikwa kwenye mabango ya waandamanaji hao, Balozi Slaa alisema unamhukumu Rais kwa mambo ambayo mahakama haijathibitisha.

Chanzo; Mwananchi


from MPEKUZI

Comments