Gwanda, Mtikila, Fatma Karume watunukiwa tuzo haki za binadamu

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), umewapa tuzo mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Mwananchi aliyetoweka, Azory Gwanda na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha DP, Christopher Mtikila kutokana na mchango wao katika utetezi wa haki za binadamu.

Gwanda ambaye kituo chake cha kazi ni Kibiti mkoani Pwani alitoweka tangu Novemba, 2017 ilhali Mtikila alifariki dunia kwa ajali ya gari katika Kijiji cha Msolwa mkoani Pwani Oktoba 4, 2015.

Mke wa Gwanda, Anna Pinoni ndiye aliyepokea tuzo hiyo kwa niaba ya mumewe, huku ya Mtikila ikipokewa na mkewe Georgia.

Wengine waliopewa tuzo na THRDC ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume na Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi (TSN), Abdul Nondo. Tuzo hizo zilitolewa katika kuadhimisha miaka mitano ya mtandao huo.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Anna alisema ingawa inamhuzunisha, lakini inatia moyo kwa sababu inadhihirisha kuna watu wanatambua mchango wa mumewe.

“Nashukuru mtandao huu kwa kuthamini kazi ya mume wangu, ninajivunia kupata tuzo hii ingawa mpaka leo sijui mume wangu yupo wapi. Ninatamani angekuwapo apokee tuzo hii, lakini naamini ipo siku atarudi na kupokea tuzo,” alisema Penina.

Kwa upande wake, mke wa Mtikila, Georgia alisema alimfahamu mumewe akiwa tayari ni mwanaharakati wa masuala ya sheria.

“Mume wangu siku zote alikuwa akiamini kuwa Katiba ni sheria mama, hakuwa adui wa Serikali, bali alipingana na Serikali kuhakikisha wananchi wanapata haki yao hasa kuhakikisha wananchi wanapata Katiba,” alisema.

Aliongeza, “Suala la kamatakamata, hasa kwa wanasiasa, kwetu sisi yalikuwa ndiyo maisha yetu. Mtikila alikuwa anakamatwa mara nyingi, wakati mwingine anawekwa (gereza la) Keko kama mahabusu kwa mwezi mzima.”

Akizungumza baada ya kupokea tuzo, Nondo ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema imemtia hamasa.

“Sikati tamaa kwa sababu nchi yoyote duniani hasa za Afrika unapotetea haki za wanyonge unakuwa adui, changamoto zinakuwa nyingi,” alisema na kuongeza: “Kukata tamaa ni kusaliti. Aluta kontinua.”

Pia aliwashukuru viongozi wenzake wa TSN kwa ushirikiano wanaompa.

Hata hivyo, Fatma hakuwapo kupokea tuzo yake na ilipokewa na ofisa wa THRDC kwa niaba yake.



from MPEKUZI

Comments