Takukuru Yawaburuza Mahakamani Wafanyakazi Ncca kwa kuisababishia serikalli Hasara ya Milioni 79

WAFANYAKAZI watano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) jana walifikishwa mahakamani kwa kosa la kuisababishia hasara serikali ya dola za Kimarekani 35,500 (sawa na Sh. milioni 79).

Watuhumiwa waliofikishwa kizimbani na kusomewa mashtaka ni Joseph Mtwala (36), John Mlambo (42), Mwahu Yunus (38), Mery Njau (38) na Catherine Edward (33).

Watuhumiwa kwa pamoja walisomewa shtaka moja na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru), Adamu Kilongozi akisaidiwa na Hamidu Simbano na Richard Jacopiyo alidai kuwa walitenda kosa hilo kati ya Desemba 25, mwaka 2013 na Juni 6, mwaka 2014.

Kilongozi alidai kuwa watuhumiwa hao wakiwa katika lango la Nabi mkoani Mara na lango kuu la Loduare mkoani Arusha walisababishia serikali kiasi hicho cha hasara wakiwa watumishi wa NCAA.

Mwendesha mashtaka huyo alisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Bernard Nganga, na kudai kuwa walifanya kosa hilo wakijua ni kinyume cha sheria.

Kilongozi aliiambia mahakama kuwa ushahidi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba ipangiwe tarehe ya kuanza usikilizwaji wa awali.

Watuhumiwa wote walikana shtaka hilo na walipewa masharti ya dhamana ya kila mmoja kuwa na wadhamini wawili kila mmoja Sh. milioni 7.9 au mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.

Hata hivyo, wadhamini hawakukamilisha masharti hayo jana, hivyo washtakiwa kupelekwa mahabusu hadi Aprili 10, mwaka huu.


from MPEKUZI

Comments