Mbowe Atuma Salamu Toka Gerezani

Viongozi sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiongozwa na Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, wamewataka Watanzania na wanachama wao wasiogope kwa sababu katika kupigania haki, demokrasia, amani na ustawi wa nchi lazima wapatikane watakaoumia kwa ajili ya wengine.

Ujumbe huo wameutoa wakiwa ndani ya Gereza la Segerea, Dar es Salaam jana ikiwa ni siku moja imepita baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuamuru viongozi hao wafikishwe mahakamani Aprili 3, mwaka huu ili kutimiza masharti ya dhamana zao baada ya juzi kudaiwa kushindwa kufikishwa kutokana na gari kuwa bovu.

Ujumbe huo wa Mbowe na viongozi wenzake ulitolewa jana na Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini na kada wa chama hicho, Dk. Makongoro Mahanga, waliopata muda wa nusu saa kuzungumza mambo mbalimbali na viongozi hao.

Selasini na Mahanga waliweka ujumbe huo katika akaunti zao za mtandao wa Facebook, pamoja na mambo mengine walisema wamewaona viongozi na haya ndiyo maneno yao: ‘Tuko imara, tuko vizuri. Wapelekeeni wenzetu ujumbe huu. Msiogope. Taifa linatutegemea. Chadema ndiyo pekee itakayobadilisha uonevu unaofanywa na watawala kwa Watanzania na kuwahakikishia demokrasia, amani ya kweli, haki na maendeleo. Tukiwa waoga tutakuwa wasaliti wa matamanio hayo ya Watanzania.’

“Wamesema pia wamepata muda mzuri wa kupumzika na kufanya retreat (tafakari ya kina. Tumemkuta Mbowe akiwa na Biblia mkononi. Amesema amesoma na karibu anamaliza Injili zote. Pia yeye pamoja na Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini leo (jana) wataadhimisha ibada ya Ijumaa Kuu kwa kuwashirikisha mahabusu na wafungwa wote wao kama watumishi wa neno la Mungu.”


from MPEKUZI

Comments