Hatimaye upelelezi kesi ya Aveva na Kaburu umekamilika.......Kesi Kuanza Kusikilizwa Aprili 5

Upelelezi katika kesi ya utakatishaji fedha, dola za Marekani 300,000 inayomkabili Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na Makamu wake Godfrey Nyange, maarufu kama Kaburu, umekamilika na itaanza kusikilizwa Aprili 5 mwaka huu.

Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga ameeleza hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kesi hiyo ilipokuja kwa kutajwa. 

 Katuga aliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa Aveva hayupo mahakamani hapo kwa kuwa ni mgonjwa amelazwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Baada ya taarifa hiyo, Wakili anayewatetea washtakiwa hao,Steven Mwakibolwa aliiambia Mahakama kuwa wapo tayari kuendelea na kwamba hali ya Aveva inaimarika ila siyo nzuri sana.

Hakimu Simba, amesema kama hali ya Aveva itakuwa imetengemaa kesi hiyo wataisikiliza mfululizo na kuongeza, kesi ilifunguliwa Juni 26, mwaka jana  na wajitahidi isikilizwe na kumalizika ndani ya miezi 12.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na mashitaka matano ya kutakatisha fedha na kughushi ambayo wanadaiwa kuwa kati ya Machi 15 na Juni 29,mwaka 2016 Dar es Salaam Aveva na Nyange kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata Dola za Marekani 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.


from MPEKUZI

Comments