Freeman Mbowe na Wenzake Wanyimwa Dhamana na Kupelekwa Rumande

Viongozi sita wa Chadema, wamenyimwa dhamana na watakaa rumande hadi Machi 29.

Hayo yameelezwa leo Machi 27, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

 Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri amesema watuhumiwa hao sita watakaa rumande hadi Machi 29 kusubiri kama Mahakama itatoa uamuzi wa dhamana au la.

Wamesomewa mashtaka hayo leo katika Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu na Wakili wa serikali Faraja Nchimbi.

Viongozi hao wamesomewa mashtaka manane ikiwamo kufanya maandamano yaliyosababisha kifo cha Mwanafunzi wa Chuo cha NIT, Akwilina Akwiline.

Washtakiwa hao wamesomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Mashauri.

Wanaolala rumande leo ni Mbowe, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa  Iringa Mjini, Peter Msigwa, Naibu Katibu Mkuu, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Mweka Hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho, Esther Matiko.

Wakili Nchimbi amedai kuwa kosa la kwanza ni kufanya mkusanyiko ama maandamano yasiyo na uhalali.

Kwa pamoja wanadaiwa Februari 16, 2018 wakiwa barabara ya Mkwajuni kwa pamoja walikusanyika kwa lengo la kutekeleza mkusanyiko ili watu waliokuwapo eneo hilo waogope kuona maandamano ya kuvunja amani.

Kosa la pili ni kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali, washtakiwa wote wanadaiwa kutenda kosa hilo Februari 16,2018 Barabara ya Kawawa maeneo ya Kinondoni Mkwajuni.

Kwa pamoja wanadaiwa wakiwa na watu wengine 12 ambao hawajafikishwa mahakamani walikuwa katika maandamano na mkusanyiko wa vurugu.

Wakili Nchimbi amedai kuwa kosa jingine linalomkabili Mbowe ni kuhamasisha chuki kwa wananchi isivyo halali.

Inadaiwa Februari 16, 2018 akiwa viwanja vya Buibui Kinondoni DSM akihutubia wakazi wa maeneo hayo na DSM alitoa matamshi ambayo yangesababisha chuki kwa Jamii.

Pia, kosa jingine linalomkabili Mbowe ni uchochezi na kusababisha chuki katika jamii, Februari 16,2018.

Inadaiwa akiwa Uwanja wa Buibui Kinondoni akihutubia alitoa matamshi  ambayo yangesababisha chuki katika Jamii.

Pia, Mbowe anakabiliwa na kosa jingine la uchochezi wa uasi, ambapo inadaiwa amelitenda Februari 16,2018 katika viwanja vya Buibui Kinondoni.

Inadaiwa akiwa na nia ya kupandikiza chuki na dharau dhidi ya uongozi uliopo madarakani alitoa maneno ambayo ni wazi yangesababisha uasi.

Pia, kosa jingine linalomkabili Mbowe ni uchochezi wa uasi, inadaiwa amelitenda Februari 16,2018 katika viwanja vya Buibui, Kinondoni.

Inadaiwa akihutubia mkutano wa hadhara alitoa matamshi ambayo yangepandikiza chuki na dharau kwa wananchi wa Tanzania dhidi ya uongozi uliopo madarakani.

Kosa la saba linamkabili Mbowe ni ushawishi wa utendeji wa kosa la jinai, ambalo amelitenda Februari 16, 2018 maeneo ya Buibui Kinondoni DSM.

Inadaiwa Mbowe akiwa amejumuika na watu wengine aliwashawishi wakazi wa maeneo hayo na kutenda kosa.

Katika kosa la nane, Wakili Nchimbi amedai linamkabili Msigwa ambalo ni kushawishi raia kutenda kosa la jinai.

Msigwa anadaiwa ametenda kosa hilo Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui Kinondoni, ambapo aliwashawishi wakazi wa maeneo hayo kutembea mbele ya umma wakiwa na silaha.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa wote walikana. Wakili Nchimbi amedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na ameomba tarehe kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.

Hata hivyo, Wakili Nchimbi aliwasilisha maombi kwa Mahakama hiyo ili washtakiwa wanyimwe dhamana kwa sababu ya usalama wa umma wa Watanzania.


from MPEKUZI

Comments