Ndugu wagoma kuchukua mwili wa Akwilina

Ripoti maalum ya uchunguzi kuhusu kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini imezua kizungumkuti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ulipohifadhiwa baada ya ndugu wa marehemu kuelezwa kuwa majibu ya ripoti hiyo yatatolewa baada ya siku 14 huku baadhi yao wakipinga jambo hilo na kutaka wapewe leo.

Wakizungumza  leo Februari 19, 2018 baada ya postmortem ya uchunguzi huo, ndugu wa Akwilina waliokuwa wamekusanyika Muhimbili karibu na eneo la chumba cha kuhifadhia maiti wakisubili ripoti, wameeleza kusikitishwa kwao na uamuzi huo huku wakilalamika na kuhoji kwa nini wasipewe ripoti hiyo leo ili wakazike mwili wa ndugu yao.

“Tumeambiwa na daktari tayari uchunguzi umeshakamilika, tuchukue mwili tukazike, lakini wanasema majibu yatatoka baada ya siku 14. Hivi tukienda tukizika tutawaambiaje waombolezaji na ndugu wengine, kwamba ndugu yetu alikufa je?” alisema ndugu mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake litajwe.

Kwa upande wa Mkuu wa  NIT, Prof. Zakaria Mganilwa amesema uongozi wa chuo hicho umeungana na familia kuhakikisha wanampumzisha Akwilina huku akifanya jitihada za kuzungumza na madaktari na ndugu wa marehemu kufanikisha zoezi la kuchukua mwili na kwenda kuuzika.

“Ripoti juu ya kifo chake madaktari wanasema itakuwa tayari baada ya siku 14 hivyo wakawa wamewaruhusu ndugu kuchukua mwili huo ili wakazike lakini ndugu wa marehemu wanasema hawawezi kuchukua mwili mpaka wajue yaani ripoti itoke ndiyo waweze kuchukua mwili kwa hiyo bado wanaendelea kufanya majadiliano na mamlaka husika,” alisema Profesa Zacharia.

 

Akwilina alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi kichwani akiwa kwenye daladala wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chadema.


from MPEKUZI

Comments