Naibu Waziri Mavunde Aagiza Wakurugenzi Kupandishwa Kizimbani Jijini Mwanza....Sababu Ziko Hapa

Khalfan Said, Mwanza
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Mhe. Antony Mavunde, (pichani juu), ameagiza waajiri ambao hawajajisajili na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kufanya hivyo, vinginevyo wafikishwe mahakamani mara moja.
 
 Mhe. Mavunde ametoa agizo hilo Jumatatu Februari 26, 2018 baada ya kufanya ziara ya kushtukiza jijini Mwanza, kubaini waajiri ambao bado hawajatekeelza takwa la kisheria kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia Kwa Wafanyakazi, Sura 263 marejeo ya mwaka 2015, ambayo inamtaka kila mwajiri kutoka sekta ya umma na binafsi Tanzania bara awe amejisajili na kuwasilisha michango kwenye Mfuko huo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko huo, Bw. Anslem Peter,  jiji la Mwanza pekee lina waajiri 1228, lakini kati ya hao ni waajiri 482 tu ndio waliojisajili na Mfuko huku waajiri wengine 746 wakiwa bado hawajajisajili. Hali hiyo ndiyo iliyomfanya Mhe. Naibu Waziri kufanya ziara hiyo ya ghafla.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mara baada ya ukaguzi huo wa kushtukiza, Mhe. Mavunde pia ameiagiza WCF kuwafikisha mahakamani mara moja, waajiri wa kampuni ya ujenzi ya JASCO, (Mkurugenzi Mtendaji Bw.Karan Bachu),

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Airco Holdings  inayotoa huduma za kusogeza vifurushi na mizigo uwanja wa ndege wa Mwanza na hoteli ya Belmonte ya jijini humo ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa Hoteli hiyo, Bw. Philemon Tei, amejikuta matatani.

"Naagiza  waajiri hao kulipa michango yote ya nyuma (tangu tarehe 1 Julai 2015 tangu Mfuko ulipoanza kutekeelza majukumu yake au siku mwajiri aliyoanza kazi zake iwapo ni baada ya tarehe 1 Julai 2015).

Mhe. Mavunde ameagiza waajiri hao kufanya mawasiliano na watendaji wa Mfuko haraka iwezekanavyo ili kuweza kubaini kiwango cha riba kila mwajiri anachopaswa kulipa kutokana na kuchelewesha michango katika Mfuko. 

“Ni kosa la jinai kwa mwajiri kutotekelza takwa hilo la kisheria na kifungu cha 71(4) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi kimeweka wazi kuwa mwajiri wa aina hii, anaweza kutozwa faini isiyozidi shilingi milioni 50,000, kifungo kisichozidi miaka 5 jela au adhabu zote kwa pamoja, kwa hivyo nitoe wito kwa waajiri hao, hakuna sababu ya kushurutishwa kutekeleza sheria.
 
"Tutatekelza agizo la Mhe. Waziri kama alivyolitoa, na nitoe rai tu kwa waajiri kote nchini (Tanzania Bara), kutekeleza takwa hilo la kisheria, kwani hakuna kichaka cha kujificha tutawafikia." Alisisitiza Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko huo, Bw. Anslem Peter katika taarifa yake kwa waandishi wa habari.


from MPEKUZI

Comments