Mwandishi: Grace Godfrey Rweyemam
Tukubali tukatae kuna adui wa kila mwanadamu, yaani ibilisi shetani. Huyu hana rafiki, hata kwa wanaompenda yeye si rafiki. Utamtumikia na kufanya mambo yake lakini mwisho wa siku hana pema pa kukupeleka zaidi ya jemanam ambayo yeye huishi huko.
Na hata utatenda mapenzi yake lakini hakuwekei ulinzi au kukuzuilia usipate mabaya, badala yake yeye mwenyewe husababisha mabaya kwako. Mungu ni upendo, na ndani yake hamna chuki. Ni shauku yake kila mwanadamu aishi kwa mapenzi na makusudi yake ili afurahie upendo wake.
Lakini alimuumba mtu kwa sura na mfano wake, hivyo ameweka utashi ndani yake. Utashi ambao mtu huwa nao ndio humpa nafasi ya kukubali au kukataa upendo wa Mungu, na hakuna namna ambayo Mungu huweza kutulazimisha tuwe vile anataka. Ameweka chaguo mbele yetu, uzima na mauti, uzima wa milele na mauti ya milele. Kwa anayechagua uzima akiwa hai huyo atauishi uzima huo hata baada ya kufa.
Najua kuna watu hawaamini kile ninachokiamini mimi, lakini hata wana sayansi huzungumza vile walivyothibitisha. Mwana historia anayesema binadamu wa kwanza aikuwa sokwe, ana vithibitisho vyake, ingawa yeye mwenyewe hakuwa sokwe kabla ya kuwa binadamu.
Kwa miaka zaidi ya ishirini kama mkristo, na hasa katika uzoefu wangu wa Mungu kuniponya na uvimbe ndani ya ubongo wangu, na changamoto nilizopitia wakati huo hata kufikia hali ya kufa, nimehakikisha jambo moja juu ya kile ninachokiamini, kuwa ni kweli Mungu yupo na anaishi ndani ya wanadamu kwa njia ya Yesu Kristo na Roho mtakatifu.
Ni Dhahiri kwa kila anayekubali na kumpokea Yesu, kama ambavyo ilitokea kwa Jovina, ndani yake hutokea badiliko la kweli la maisha. Haingekuwa rahisi binti huyu ambaye ndani ya miaka sita amekuwa chini ya kifungo cha mume mchawi kurudi nyumbani kwake kwa ujasiri huku akijua ameshaharibu kazi za mumewe.
Kwake yale maombi hayakuwa tu muujiza wa mtoto wake kulindwa asiuliwe na mumewe kama ambavyo awali alidhani, bali yalikuwa maombi yenye badiliko kwa maisha yake kwa ujumla. Mchungaji alimuongoza maombi baada ya kumuelewesha kuhusu yeye binafsi kufanya uamuzi wa kumkubali Kristo.
Mara nyingi tumekutana na changamoto na tukaamua kumtafuta Mungu ili kupata suluhisho la changamoto zetu, lakini mtu anayenunua ndoo ya maji kuna siku yatamuishia, na ni bora kwake angechimba kisima. Kuwa na Kristo ni sawa na kisima cha maji yasiyokauka, na hicho ndicho ambacho kila mtu huhitaji.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment