Mpenzi Wangu Ibilisi ( Simulizi ya Kweli) Sehemu ya 02

Mwandishi: Grace Godfrey Rweyemam

Mume wangu ni hodari sana wa kuonyesha mapenzi na ingawa hufuata kwa umakini masharti yake kwamba mimi nisionekane kama mke wa tajiri, lakini kiukweli alinionyesha mapenzi ya dhati. Alinisifia na kunisaidia hadi kazi za ndani kwani hakutaka tuishi na binti wa kazi.

Tulikuwa na wafanyakazi wawili waliokuja na kuondoka ila mara kadhaa aliwaambia wasije wapumzike. Naweza kuhesabu ni mara ngapi nimepika kwani mara nyingi sana mume wangu hupika, hufua mpaka nguo zangu za ndani, na hata kuniogesha.

Watoto wakiwa katika umri wa kuhudumiwa na mzazi mara zote yeye ndiye huwahudumia, bila shida yoyote, yaani hata kuamka usiku. Mwanzoni nilikuwa naona ni vitu vya ajabu au labda anafanya hivyo kunisahaulisha alichoniambia lakini mpaka leo hii ni mwaka wetu wa sita na hajabadilika, kiasi cha kunifanya mimi niwe mvivu wa kazi.

Nilipoendelea kuishi naye nilianza kugundua vitu vya ajabu, na wewe ni mtu wa kwanza kabisa ninakwambia. Sijui kwanini nimeamua kukutafuta nikwambie, na sielewi ni wapi nimepata ujasiri mkuu namna hii, lakini nikifuatilia ushuhuda wako, nilianza kushawishika kuwa unaweza kunisaidia. Sitaweza kukueleza kwa kirefu kuhusiana na uchawi wa mume wangu, lakini kwa kifupi ni mchawi mkubwa sana hapa nchini.

Huua watu wengi na ameshawaua hata wazazi wake mwenyewe, na ninavyokwambia sio kwamba nimehadithiwa bali yeye mwenyewe amewahi kukiri kwa kinywa chake kuwa ndiye aliyeua wazazi wake.

Nyumbani kwangu nimeshakutana na vitu vingi vya ajabu. Ninavyokwambia, nimeshawahi kuona kwa macho yangu damu na nyama za watu kwenye frij yake maalumu nyumbani ambayo alinizuia kuigusa, halafu siku moja akasahau funguo. 



from MPEKUZI

Comments