Meli nyingine 19 zapigwa faini ya mabilioni na Serikali

Na John Mapepele
Serikali imezipiga faini ya bilioni kumi na tisa  meli 19 ikiwa ni shilingi bilioni moja kwa kila meli na kuamuliwa kulipa faini hiyo ndani ya wiki mbili kwa kukiuka kanuni ya 10 ikisomeka pamoja na kanuni ya 68 ya kanuni za uvuvi wa Bahari Kuu za mwaka 2009 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016 kwa kutoripoti katika bandari Dar es Salaam, Zanzibar, Mtwara ama Tanga kwa ajili ya ukaguzi kabla ya kutoka katika bahari kuu ya Tanzania.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, katika Ofisi za Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari  Kuu zilizopo Fumba kisiwani Unguja, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Joelson Mpina  amesema pamoja na meli hizo kuamriwa kulipa faini ya Shillingi Billioni moja (Tshs. 1,000,000,000) kila moja zinatakiwa  kurejea katika bandari za Tanzania kwa ajili ya ukaguzi kwa kuwa leseni zao bado hazijaisha muda wake hadi sasa ili kubaini thamani halisi ya kiasi cha fedha zitakazotozwa kwa ajili ya samaki waliovuliwa bila kukusudia(Bycatch).

Aidha Mpina amesema  meli hizi zimetakiwa kuilipa Tanzania kiwango cha pesa kwa mujibu wa soko la kimataifa kutokana na kuondoka na Bycatch waliyoripoti kuwa wanayo kabla ya kutoroka.

Waziri Mpina amemuagiza Katibu Mkuu Uvuvi, Dkt. Yohana Budeba  kuiamru Mamlaka ya uvuvi wa Bahari Kuu (DSFA) iwaandikie notisi wahusika wa meli hizi kuwajulisha kuhusiana na maamuzi haya pia kuwajulisha Kamisheni ya Jodari kwenye Bahari ya Hindi, (IOTC) kuhusiana na hatua zilizochukuliwa na Tanzania dhidi ya meli hizo ili isaidie kuwabaini na kuwachukulia sheria kwa mujibu wa Sheria husika.

Aidha imeamriwa kwamba Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu pia iandae barua/ andiko kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili aweze kuiandikia Barua Wizara ya Mambo ya Nje kwa lengo la kuwasiliana na Flag States (Mataifa ambayo meli hizi zimesajiliwa) ili kuwajulisha makosa yaliyotendwa na meli husika pamoja na hatua ambazo Tanzania imechukua. Amesema meli zote zilizotoroka zimesajiliwa nchini China.

Wakati huo huo Waziri Mpina amesema  meli ya Tai Hong 1 imekiuka Kifungu cha 18 cha Sheria ya uvuvi wa Bahari kuu No. 1 ya Mwaka 1998 na marekebisho yake ya mwaka 2007 pamoja na Kanuni ya 66 ya kanuni za uvuvi wa Bahari kuu za Mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2016 kwa kukutwa na mapezi ya papa yasiyoendana na miili iliyokutwa kwenye meli hiyo baada ya kukaguliwa katika bandari ya Dar es Salaam mnamo tarehe 25/01/2018-27/01/2018. 

Pia meli hii imebainika kukiuka kanuni ya 10 ikisomeka pamoja na kanuni ya 68 ya kanuni za uvuvi wa Bahari Kuu za mwaka 2009 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016 kwa kuhaulisha mabaharia kutoka kwenye meli nyingine ambao idadi yao ilikuwa mabaharia 10.

Aidha meli hii pamoja na kukutwa na makosa hayo iliondoka nchini bila kufuata taratibu zinazotakiwa kwa mujibu wa vifungu tajwa hapo juu.

Kutokana na makosa hayo imeamriwa na Mamlaka ya Bahari kuu (DEEP SEA FISHING AUTHORITY) kulipa jumla ya faini ya Shillingi Billion moja (Tshs. 1,000,000,000) ambapo Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu itawasilisha notisi ya adhabu hii kwa wahusika wa Meli hii ya TAI HONG 1.

Mbali na Tai Hong 1 Mpina amezitaja Meli hizo zilizopigwa faini ya Bilioni moja kila moja kuwa ni pamoja na TAI HONG NO2 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/453, TAI HONG 8 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/454, ,TAI XIANG 2 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/455, TAI XIANG 5 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/456, TAI XIANG 1 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/457, TAI XIANG 8 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/458 na TAI XIANG 9 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/459.

Meli nyingine ni TAI XIANG 10 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/460, TAI XIANG 7 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/461, TAI XIANG 6 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/462,  TAI HONG 6 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/463,  TAI HONG 7 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/464, XIN SHIJI 81 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/466, XIN SHIJI 82 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/467, XIN SHIJI 83 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/468, XIN SHIJI 86 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/470, XIN SHIJI 72 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/471, XIN SHIJI 76 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/472 na JIN SHENG 1 yenye  namba ya leseni TZ/DSFA/EEZ/473.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Yohana Budeba amewataka wawekezaji kwenye  bahari ya Tanzania kuwa waaminifu na kuzingatia masharti na taratibu za kisheria  ili nchi na wawekezaji waweze kunufaika.

“Taratibu zipo wazi ni muhimu  kuzinangatia sheria  namna nyingine tutaendelea kusimamia sheria za nchi yetu kwa faida ya sasa na vizazi vya baadaye” Alisisitiza Dkt. Budeba

Amesema  hatua iliyochukuliwa na Serikali  ya kuzipiga faini meli hizo ni somo kwa meli nyingine na kwamba Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa yoyote atakayebainika kutenda  makosa  ya uvuvi haramu katika bahari na maziwani.

Aidha amesema Serikali ipo tayari kufanya biashara  na mtu yoyote ambaye atazingatia masharti ya nchi, na kwamba taifa linajipanga ili kuwa na makampuni yake ya TAFICO na ZAFICO yatakayoshuhulika na uvuvi ili kunufaika na raslimali za uvuvi kama ambavyo inafanyika katika nchi mbalimbali duniani.

Amesema hatua hiyo itasaidia kukuza ajira kwa wananchi, uchumi wan chi na kuanzisha viwanda vya kuchakata samaki na mazao yake.

Aliwashukuru  wadau wote wanaoshiriki kwenye mapambano ya uvuvi ambapo kipekee alilishukuru shirika lisilo la kiselikali la Sea worrior kwa kutoa mchango mkubwa kwenye operesheni Jodari ambayo imefanywa  na wadau mbalimbali nchini.


from MPEKUZI

Comments