Matokeo Ya Uchunguzi Kuhusu Kauli Ya Askofu Zachary Kakobe

Kufuatia kauliiliyotolewa na Askofu Zachary Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship katika mahubiri ya Ibada ambayo alisema kuwa “Yeye ana pesa kuliko Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilifanya uchunguzi ili kubaini usahihi wa kauli hiyo.

Yafuatayo ni mambo ambayo yalibainika baada ya kufanyika uchunguzi kuhusu kauli ya Askofu Zachary Kakobe;

1.Askofu Zachary Kakobe hana akaunti wala fedha katika taasisi yoyote ya fedha hapa nchini. Aidha uchunguzi ulibaini kuwa Askofu Kakobe ni mmoja wa wasimamizi wakuu wa akaunti za kanisa (signatories) zilizopo katika benki ya NBC zenye jumla ya kiasi cha shilingi 8,132,100,819.00, kiasi hiki cha fedha kimetokana na sadaka, zaka na changizo ambazo zinatolewa na waumini wa kanisa tajwa hapo juu, hivyo kwa mujibu wa Sheria hakitozwi kodi.

2.Kanisa lilikwepa kulipa kodi kiasi cha shilingi 20,834,843.00 ambazo zilitokana na uwekezaji katika makampuni ya kukuza mitaji.Kodi hiyo imelipwa baada ya uchunguzi.

3.Kampuni inayomilikiwa na watoto wa Askofu Zachary Kakobe ilikwepa kulipa kodi kiasi cha shilingi 37,280,030.00 ambazo zimelipwa baada ya uchunguzi. Kwa ujumla, kiasi cha kodi kilicholipwa kutokana na uchunguzi huu ni shilingi 58,114,873.00.

4. Kanisa linatunza kiasi kikubwa cha fedha kwenye ndoo na ‘majaba’ kinyume na taratibu za utunzaji wa fedha, lakini pia uwekaji na utoaji wa fedha nyingi kutoka benki haushirikishi vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya usalama wa fedha zenyewe na wahusika.

5.Pia ilibainika kwamba Kanisa halitengenezi hesabu za Mapato na Matumizi ya Fedha kitu ambacho ni kinyume na Katiba ya Kanisa pamoja na sheria za usimamizi wafedha ambayo imepelekea matumizi mabaya ya fedha za waumini kama vile safari za nje ya nchi ambazo zimedhaminiwa na Kanisa lakini wanaosafiri ni Askofu na familia yake.  Vile vile fedha za Kanisa zinatumika kujenga nyumba ya mke wa Askofu, kwa jina lake na wala si kwa jina la Kanisa, kitu ambacho ni kinyume na taratibu za Kanisa.

Aidha, wakati uchunguzi huo ukiendelea,mnamo tarehe 24.01.2018 Askofu Kakobe aliandika barua kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuomba radhi kutokana na kauli yake ya kebehi pamoja na matamshi yake ya dharau kwamba ana pesa nyingi kuliko Serikali.

WITO:
•  Mamlaka ya Mapato Tanzaniainatoa wito kwa Taasisi zote za dini ambazo zinajihusisha na shughuli zozote za kiuchumi kulipa kodi stahiki na kwa wakati kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kodi.

• Mamlaka ya Mapato Tanzania inazitaka Taasisi zote za kidini kufuata katiba zao ikiwa ni pamoja na kutengeneza hesabu za mapato na matumizi.

Charles E. Kichere
KAMISHNA MKUU 
MAMLAKA YA MAPATO TANZANIA

“Pamoja Tunajenga Taifa Letu”


from MPEKUZI

Comments