Upande wa utetezi katika kesi ya kughushi, inayomkabili mfanyabiashara, Hussein Shabani maarufu ‘Ndama mtoto wa Ng’ombe’ umeuomba upande wa mshtaka kuifuta kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hadi upelelezi utakapokamilika.
Hayo yameelezwa leo February 28 na Wakili wa utetezi Jeremia Ntobesya mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Victoria Nongwa, baada ya wakili wa serikali Christopher Msigwa kudai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.
Pia Msigwa amedai kuwa wameongea na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuandikiwa taarifa kwa sababu kesi hiyo ni ya muda mrefu.
Msigwa ameeleza kuwa sehemu ya upelelezi iliyobakia ni kutoka nje ya nchi na kwamba wanatambua haki ya mshtakiwa na wanafanya juhudi za ziada na ikishindikana watafanya maamuzi.
Kutokana na hoja hizo, wakili wa Ndama, Ntobesya amedai kuwa mshtakiwa ana haki ya kuwa huru, hivyo anauomba upande wa mashtaka kufuta kesi hiyo hadi pale watakapomaliza upelelezi, kisha waifungue tena kesi hiyo.
Kutokana na hoja hizo, Hakimu Nongwa ameahirisha kesi hiyo hadi March 27,2018 kwa ajili ya kutajwa.
Ndama anakabiliwa na mashtaka matano ambapo anadaiwa kuwa February 20, 2014 Dar es Salaam, alighushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha maboxi manne ya dhahabu yenye kilogramu 207 yenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000.00 kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.
Pia anadaiwa March 6, 2014, Dar es Salaam, alighushi kwa kutengeneza hati ya kibali ya Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam akijaribu kuonesha kilogramu 207 za dhahabu kutoka nchini Congo zinatarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited, zimesafirishwa bila jinai yoyote wakati akijua si kweli.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment