Hatimaye Ndugu Wamekubali Kuuchukua Mwili wa Mwanafunzi Aliyepigwa Risasi

Ndugu wa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline aliyepigwa risasi na Polisi Februari 16, 2018 wameeleza ndugu yao alifariki dunia baada ya kupigwa risasi kichwani.

Wametoa ufafanuzi huo leo Februari 19, 2018 muda mfupi baada ya kususa kupokea mwili wa mwanafunzi huyo uliokuwa ukifanyiwa uchunguzi Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) bila kuelezwa nini kilichomuua.

Wakizungumza mara baada ya maafikiano baina yao na madaktari, wamesema wamepewa sehemu ya ripoti ya uchunguzi ambayo wameridhika nayo na sasa wanakwenda kufanya kikao cha ndugu kujadili namna gani watampumzisha Akwilina.

Shemeji wa mwanafunzi huyo, Festo Kavishe amesema uchunguzi wa mwili huo, umeonyesha kwamba Akwilina alijeruhiwa vibaya kichwani.

"Ripoti ambayo tumepewa imeonyesha kwamba kichwa cha marehemu kilipasuliwa vibaya na risasi ambayo iliingilia upande wa kushoto kwa kichwa chake na kutokea upande wa kulia  ambao umefumuka vibaya," amesema.

Kwa mujibu wa Kavishe, iwapo madaktari wasingewapatia majibu hayo wasingethubutu kuuchukua mwili huo kwa mazishi, kwa sababu walihitaji kupata picha kamili ya nini kilimuua Akwilina.

"Sasa tumeshafahamu nini hasa kimemuua ndugu yetu kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na madaktari baada ya uchunguzi, hivi sasa tunakwenda kujadiliana kuhusu mazishi yake," amesema Kavishe.

Akwilina alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi kichwani akiwa kwenye daladala wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji ambao ni wafuasi wa Chadema.


from MPEKUZI

Comments