Wanachama wahofia kufilisiwa shamba, wampigia magoti Rais Magufuli

Wanachama wa chama cha Ushirika cha Uru Kati Mawela, wamemuomba Rais John Magufuli, kuingilia kati mgogoro wa ardhi wakihofia kufilisiwa shamba walilopewa na Serikali lenye ukubwa wa hekari 213.

Wasiwasi huo unatokana na kushindwa kesi waliyoifungua dhidi ya kampuni ya mwekezaji, Laitolya Tours & Safaris, ambayo imejenga hoteli ya kitalii ya Kilemakyaro Mountan Lodge ndani ya hekari 27.54.

Hayo yamejitokeza katika mkutano mkuu maalum wa wanachama ulioitishwa jana Januari 27, mahsusi kujadili hukumu hiyo iliyotolewa Ijumaa ya Januari 19 na Jaji Benedict Mingwa wa Mahakama Kuu Moshi.

Katika hukumu hiyo, Jaji Mingwa amesema  hekari hizo 27.45 ni mali ya Laitolya Tours and Safaris na kuutaka ushirika huo kukabidhi hati namba CT10663 ili kampuni imilikishwe hekari hizo 27.54.

Mbali na kuamuru hati hiyo ikabidhiwe kwa msajili wa hati, lakini Jaji Mingwa ameamuru pia kuwa wana ushirika hao watalazimika kulipa gharama za kesi hiyo ya madai namba 10 ya mwaka 2015.

Hata hivyo, Mrajisi Msaidizi wa vyama vya Ushirika mkoa Kilimanjaro, Henjewele John, ameliwaambia wanachama hao kuwa mwekezaji huyo amempibu Rais Magufuli na kwamba atampigia simu.

“Niwaahidi kwamba tutatumia njia zote kuhakikisha kuwa wananchi wa Uru wanapata haki yao. Hapa tutamwambia Ushirika leteni hati yenu ya kumiliki na huyu mwekezaji alete hati zake,”amesema.

“Sasa hivi nataka niwaambie majumba ya watu yanabomolewa. Si mnaona? Kwa hiyo huyu mzee wetu amebipi sasa akibipu sisi tutapiga. Zama zimebadilika na kwa hili tutalifikisha kwa Rais,”amesisitiza.

Mwenyekiti wa Ushirika huo, Richard Kimaro, amesema wao hawakuwahi kumpa mwekezaji huyo eneo hilo la ardhi, bali walimkodishia lakini aliwazunguka kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi.

“Katika kipindi chote cha mkataba tangu 1998 hakuwahi kulipa kodi ya pango ambayo kwa mujibu wa mkataba ilikuwa Dola 700 za Marekani (sawa na Sh1.6 milioni) kwa mwezi,”alidai mwenyekiti huyo.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, ni kutokana na kutolipa kodi hiyo na kujimilikisha ardhi yao, walifungua kesi ya madai wakitaka ushirika ulipwe malimbikizo ya kodi yanayofikia Dola 153,600.

Mbali na kudai fedha hizo, lakini waliiomba mahakama itamke kuwa mwekezaji huyo ni mvamizi na ameingia kwa jinai katika shamba lao na pia imuamuru alipe fidia ya jumla ya Sh80 milioni.

Akizungumza katika mkutano huo, mmoja wa wanachama wa Ushirika huo, Francis Moshi, alisema wamekanganyikiwa waliposikia wameshindwa kesi na kudaiwa kuwa wao ndio walivuruga mkataba.

“Tunajiuliza hivi ni nani hapa alivuruga mkataba kati yetu na Laitolya ambaye hakulipa kodi ya pango kwa mujibu wa mkataba? Ulikuwa mkataba wa miaka 10 akaongeza sifuri ukawa miaka 100,”amedai.

Makamu Mwenyekiti wa Ushirika huo, Emanuel Mushi, alisema kilichojificha ni kuwa baadhi ya viongozi walishiriki kughushi muhtasari wa vikao mbalimbali kwa maslahi ya mwekezaji huyo.

Wajumbe wa mkutano huo waliazimia kwa kauli moja, kwamba bodi ya uongozi ya chama hicho ikate rufaa kupinga hukumu hiyo na pia ilipeleke suala hilo ngazi za juu Serikalini kupitia kwa Mrajisi.

Hata hivyo mkurugenzi wa kampuni hiyo, Joachim Minde alipotafutwa jana, alisema anawashangaa wanachama hao kufanya mkutano badala ya kukata rufaa kama hawakuridhika na uamuzi.

“Wao kama wanataka kwenda kwa Rais sijui Waziri wa Ardhi wao waende. Kama mimi nina haki yangu si lazima nitalalamika? Wao kama nao wanaona wana haki walalamikie mahakama,”amesema.

“Huwezi kulalamika kuwa unamtaka Rais sijui unamtaka Waziri. Hili jambo sio la leo. Alishakuja Waziri wa Ushirika na pia akaja Waziri wa Ardhi hapa. Sio jambo geni kabisa,”amesisitiza Minde.

Minde amedai kuwa kinajitokeza ni kwamba wamekuja baadhi ya viongozi wa Ushirika ambao ni wageni wanaosumbuliwa na njaa na atafurahi sana kama siri ya mgogoro mzima ujulikane.

Mkurugenzi huyo alisema huu ni wakati wa kujua mapato na matumizi ya shamba hilo na kwamba kwa sasa anajiandaa kufungua kesi nyingine ya madai kwa jinsi walivyopata hasara tangu 1998.


from MPEKUZI

Comments