Tundu Lissu Atolewa Risasi Nyingine Mwilini Mwake

Siku 35 baada ya Tundu Lissu kusema mwili wake bado una risasi moja baada ya kutolewa nyingine 15, jana mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema) alisema kuwa madaktari wamemtoa kipande cha risasi kilichokuwa mwilini mwake.

Hata hivyo, mwanasheria huyo mkuu wa Chadema, ambaye alishambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 akiwa ndani ya gari lililokuwa nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7 mwaka jana, alisema chuma hicho ni tofauti na risasi aliyonayo mwilini, ambayo alielezwa na madaktari wa Hospitali ya Nairobi, Kenya kuwa iko sehemu mbaya, lakini isipotolewa haiwezi kumdhuru.

“Leo (jana) madaktari wamenitoa kipande cha chuma katika sehemu ya makalio ambacho nilipokuwa Nairobi (Kenya) madaktari walikiona lakini kilikuwa ndani ya nyama wakashindwa kukitoa,” alisema Lissu

“Kipande hiki kilisogea na wamekitoa. Ni tofauti na ile risasi ambayo iko mwilini mwangu.”

Akieleza kiundani kuhusu hali yake, Lissu alisema anaendelea vizuri.

“Huu mkono wa kushoto ambao ulikuwa na tatizo, wameunyoosha na kuufanyia mazoezi kweli kweli na huu mguu wa kulia ambao ndio wenye tatizo, unaendelea vyema,” alisema.

“Huku ni mazoezi tu. Kwa siku nafanya mazoezi kwa saa nne, Naingia saa 3:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi, narudi tena saa 5:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana. Mwisho naingia mazoezini saa 8:00 mchana hadi saa 10:00 jioni. Hiyo ndiyo ratiba yangu kwa siku.”

Alisema katika mazoezi hayo anatumia magongo maalumu pamoja na kiti cha magurudumu.

“Mfano, huu mguu wa kulia natakiwa kuukanyagia kwa kilo 20 hadi 25 katika mzani na mimi nina kama kilo 90. Ninapoukanyagia ninaulizwa kama unauma, ikiwa sijasikia maumivu ina maana sijafanya kitu, kwa hiyo ni kazi kwelikweli,” alisema.

Kuhusu muda ambao anatakiwa kufanya mazoezi hayo mpaka atakaporejea katika hali yake ya kawaida, Lissu alisema bado hajajua.

“Ah bwana we, hapa madaktari wamegoma kunieleza hilo, lakini wameangalia katika maungio ya goti la mguu wa kulia kuna mfupa haujaunga vizuri, ni lini utaunga hilo sijajua,” alisema.

Mara baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya siku hiyo usiku.

Desemba 21 mwaka jana wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha Azam, Lissu alisema madaktari wa Nairobi walimueleza kuwa risasi iliyokuwa imesalia mwili haina madhara.

Alisema risasi saba zilitolewa na madaktari hao, jambo lililomaanisha kuwa risasi nyingine nane, zilitolewa na madaktari wa Tanzania, saa chache baada ya kushambuliwa alipofikishwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.    


from MPEKUZI

Comments