Madiwani Watatu wa CHADEMA Kilimanjaro Watimkia CCM

Katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Rombo, Katibu wa NEC Mwenye dhamana ya Itikadi na Uenezi Ndg. Humphrey Polepole ameujulisha umma wa wananchi wa Rombo kuwa baada ya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani na kutambua uwepo wa kero kubwa ya Maji, amewasiliana na Uongozi wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji na kwamba ukosefu wa kiasi cha shilingi Milioni 130 kilichokuwa kinakosekana ili kufanya upembuzi yakinifu wa mradi wa kuvuta maji kutoka Ziwa Chala sasa zitatolewa na Wizara ili tatizo la upungufu mkubwa wa maji Wilaya ya Rombo limalizike.

Aidha Ndg. Polepole akawaelekeza watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kufanya mawasiliano ya haraka na Wizara ya Maji na Umwagiliaji ili kupata fedha hizo na kuhakikisha mchakato wa kuvuta maji kutoka Ziwa Chala unaanza maramoja.

Wakati Kikao Cha Halmashauri Kuu ya Wilaya na Katibu wa Nec Itikadi na Uenezi kikiendelea madiwani watatu wa Chadema walifika eneo la kikao na kuomba wapewe fursa ya kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Pamoja na maelezo waliyoyatoa Madiwani hao wa Chadema katika kikao Cha Halmashauri Kuu ya Wilaya juu ya sababu zilizopelekea kujitoa kwao Chadema na kujiunga na CCM, wameelezea pia siri ya kudorora kwa Maendeleo Wilaya ya Rombo kuwa ni mpasuko uliopo kati ya Madiwani wanaomwunga mkono Mbunge wa Jimbo la Rombo Ndg. Joseph Selasini na madiwani wanaomwunga mkono Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo Ndg. Evarist Silayo sababu ikiwa ni vita ya Ubunge mwaka 2020.

Kikao cha Halmashauri Kuu ya Wilaya ya Rombo kwa kauli moja wamewapokea wanachama hao wapya na Ndg. Polepole akaelekeza uongozi wa Wilaya kuwapitisha katika program ya mafunzo ya Imani, Itikadi, Siasa, Masharti ya Mwanachama, Ahadi za Mwanachama na Sera za Maendeleo za CCM.

Madiwani waliojitoa CHADEMA na kujiunga na CCM leo ni Ndg. Juliana Malamsha na Martha Ushaki wa Viti Maalum pamoja na Frank Lubega wa kata ya Kelamfuamokala.

Huu ni muendelezo wa ziara za ujenzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuhuisha dhana ya Chama kushika hatamu na kuhakikisha kinaisimia Serikali katika kushughulika na shida za wananchi.

Imetolewa na,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM), ROMBO, KILIMANJARO


from MPEKUZI

Comments