LIVE UPDTES: Hali Ilivyo Kenya, 'Raila Odinga Akijiapisha Kuwa Rais'....Matangazo ya TV Yamezimwa

Hali ya wasiwasi imetanda nchini Kenya baada ya kiongozi mkuu wa upinzani nchini humo Bwana Raila Odinga, kushikilia kuwa ataapishwa leo kama rais wa nchi hiyo.

Muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) umesema hafla hiyo itafanyika katika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi.

Baada ya sherehe hizo kuahirishwa mwezi uliopita, muungano mkuu wa upinzani nchini humo-NASA, bado unaendelea na msimamo wake wa kuwaapisha viongozi wake Raila Odinga na Stephen Kalonzo Musyoka, kama Rais na Makamu wa rais wa Jamhuri ya Kenya.

Maafisa wa polisi walifika asubuhi na mapema katika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi unaopanga kutumiwa na muungano wa Nasa kwa shughuli ya kumuapisha Bw Odinga.

Kituo cha habari cha kibinafsi cha Citizen kimeripoti kuwa maafisa wa polisi wameamrishwa kuondoka katika uwanja wa Uhuru Park.

==>Mabasi ya wafuasi wa upinzani yazuiwa Voi
Mabasi matatu yaliyokuwa yanawasafirisha wafuasi wa upinzani waliokuwa wanaelekea Nairobi kuhudhuria sherehe ya kuapishwa kwa kiongozi wao Raila Odinga yamekamatwa na maafisa wa polisi katika mji wa Voi, katika barabara ya kutoka Mombasa kwenda Nairobi.

Mji wa Voi unapatikana takriban kilomita 330 mashariki mwa mji huo mkuu wa Kenya.

Afisa wa polisi amewaambia wanahabari kwamba madereva wa mabasi hayo walikuwa wamevunja sheria kadha za barabarani.

Wafuasi wa upinzani nchini Kenya wameanza kuingia uwanja wa Uhuru Park baada ya polisi kuondoka.Baadhi wanazunguka uwanja huo wakiimba ‘Uhuru Must Go’.
 
==>Wafuasi wa upinzani waliozuiliwa Voi waachiliwa
Wafuasi wa upinzani waliokuwa wanasafiri kuelekea Nairobi ambao walizuiliwa awali mjini Voi baadae wameachiliwa na kuruhusiwa kuendelea na safari.

==>Vituo vya habari vyafungiwa matangazo Kenya
Baadhi ya vituo vya redio na televisheni vya Royal Media Services (RMS), vikiwemo runinga ya Citizen TV, vimefungiwa matangazo pamoja na kituo cha televisheni cha NTV kinachomilikiwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG) katika baadhi ya maeneo.

Vituo hivyo vimekuwa vikipeperusha matangazo kuhusu sherehe iliyopangiwa kufanyika leo ya kuapishwa kwa kiongozi wa upinzani Kenya Raila Odinga.

Serikali ilikuwa imetahadharisha vituo vya habari Kenya dhidi ya kupeperusha moja kwa moja hafla hiyo.

Mmoja wa wahariri wakuu wa Citizen Peter Opondo amesema  kwamba maafisa wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA)  wakiandamana na polisi walivamia vituo vya kupeperushia matangazo na kuzima matangazo.

Citizen TV ndicho kituo cha runinga kinachoongoza Kenya. Matangazo ya kituo cha NTV yanapatikana pekee kupitia ving’amuzi vya kulipia. Kituo kingine kikubwa KTN bado kinarusha matangazo.


from MPEKUZI

Comments