Tanzania Yapokea Chanjo Ya Uviko-19 Aina Ya Sinopharm Dozi Milioni Tatu


Na. WAF – Dar es Salaam

Tanzania imepokea chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinopharm dozi Milioni tatu (3,000,000) ambazo zitawasaidia kuwakinga wananchi 1,500,000 dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa virusi vya Korona.

Chanjo hizo zimepokelewa Julai 14, 2022 na Kaimu Mkurugenzi wa Kinga Dkt. Beatrice Mutayoba wakati wa mapokezi ya chanjo hizo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dar es Salaam kutoka Jamhuri ya Watu wa China.

“Chanjo hizi zimetolewa kwa hisani ya mke wa Rais wa China Prof. Peng Liyuan, kwa niaba ya Serikali yetu nitoe shukrani sana kwa Serikali ya China hususani katika kujali Afya za watanzania kwa kutupatia chanjo hizi.” Amesema Dkt. Beatrice

Amesema hadi kufikia Julai 12, 2022 jumla ya dozi 21,226,520 zimepokelewa kutoka shirika la COVAX pamoja na nchi wahisani na tayari zimeshasambazwa katika maeneo yote nchini.

“Kuna Mikoa ambayo imezidi asilimia 30 ya utoaji wa huduma za chanjo ikiwemo Dar es Salaam lakini pia kuna Mikoa ambayo haijazidi asilimia 20 hivyo niwaombe mkaongeze juhudi za kutoa elimu kwa watanzania ili tuendelee kuwakinga na UVIKO-19. ” Amesema Dkt Beatrice

Dkt. Beatrice amesema kuwa wagonjwa wanaolazwa kutokana na kupata virusi vya Korona wengi wao wanakuwa hawajapata chanjo ya UVIKO-19 kutokana na takwimu zilizofanywa na wizara ya Afya.

Aidha, amewasihi watanzania wote wenye umri kuanzia miaka 18 kama inavyoshauriwa na wataalamu wa Afya kwenda kupata chanjo ya UVIKO-19 kwakuwa chanjo hiyo ni salama na haina madhara na kuendelea kuchukua tahadhari zote za kinga dhidi ya ugonjwa huo wa virusi vya Korona.

Kwa upande wake mwakilishi wa Balozi wa China Bw. Salim Chu Kun ametoa pongezi kwa Serikali ya Tanzania kupitia wizara ya Afya kwa kuendelea kujali Afya za watanzania wote hususani wakina mama na ameahidi kuendelea kuisaidia Tanzania na mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Naye,Mkurugenzi wa masuala ya jinsia na wanawake kutoka wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Bi. Grace Mwangwa ameishukuru wizara ya Afya kwa kutambua uwepo wao na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano katika masuala ya Afya kwa kuwa tunajenga nchi moja.

Serikali kupitia wizara ya Afya iliidhinisha matumizi ya chanjo aina ya Janseen, Pfizer, Moderna, Sinopharm, Sinovac, na Covaxin baada ya kujiridhisha na vigezo vya ubora, usalama na ufanisi kwa matumizi ya watanzania kuanzia umri wa miaka 18 na kuendelea.

Katika mapokezi hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka wizara ya Afya akiwepo Meneja mpango wa Taifa wa chanjo Dkt. Florian Tinuga na Mganga mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume.



from MPEKUZI

Comments