Serikali imesema inatambua mchango wa mafundi sanifu nchini katika kuufikia uchumi wa kidijitali unaokwenda sambamba na matokeo ya ubunifu na mabadiliko ya teknolojia.
Ameyasema hayo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Barabara Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Alois Matei, wakati akifungua Kongamano la Nne (4) la mafundi sanifu ambapo Mhandisi Matei alimwakilisha Katibu Mkuu wa Sekta hiyo, Balozi Aisha Amour.
Mhandisi Matei aliwataka mafundi sanifu nchini kuwajibika katika taaluma zao ili kuiwezesha serikali kufikia azma yake katika ukuaji wa uchumi wa kidigitali na kuepuka kupitwa na wakati na hatimaye kutupwa nje ya mfumo huo mpya.
Hivyo, akiwataka kutumia kongamano hilo na mada zitakazowasilishwa ambazo ni ubunifu wa kihandisi, mapinduzi ya nne ya viwanda pamoja na uchumi wa kidijitali katika kukuza maendeleo ya taaluma zao na namna ya kutatua matatuzo wanayokutana nayo.
“Uchumi wa kidijitali, ubunifu na mapinduzi ya nne ya viwanda vina mchango mkubwa katika kurahisisha na kupunguza gharama za utekelezaji wa kazi na miradi mbalimbali”, alisema Mhandisi Matei.
Alisema kasi ya kidugitali inagusa sekta zote za kiuchumi nchini kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani, hii ikiwa namna Watanzania wanavyopata huduma za Serikali, wanavyolipia huduma na wanavyofanya kazi.
“Mchango wenu ni mkubwa katika utekelezaji wa mipango ya Serikali ikiwemo ujenzi na uendeshaji wa mitambo, viwanda mbalimbali na miundombinu”, alisema Mhandisi Mtei.
Awali akitoa taarifa ya kumkaribisha mgeni rasmi, Msajili wa Bodi ya Wahandisi (ERB), Mhandisi Benard Kavishe, alisema kuwa bodi hiyo ilianza kusajili mafundi sanifu hao mwaka 2014 na hadi sasa imesajili jumla ya mafundi sanifu 1979.
Alisema idadi hiyo bado ni ndogo kwani kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) viwango vya uwiano wa kazi za uhandisi ni 1:5:25 ambayo ni kila mhandisi mmoja anafanya kazi na mafundi sanifu watano na chini yao mafundi stadi 25.
Kongamano hilo lililoratibiwa na Bodi ya Wahandisi Nchini limehusisha mafundi sanifu, wabunifu na mafundi mchundo zaidi ya 500 lilikuwa na kaulimbiu isemayo ‘Ubunifu wa Kihandisi, Mapinduzi ya Nne ya Viwanda na Uchumi wa Kidijitali’.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment