Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ameipongeza Taasisi ya Maendeleo ya Aga Khan (AKDN) kwa mchango wake mkubwa katika kukuza na kuendeleza sekta za elimu, afya, miundombinu, utalii na utamaduni hapa nchini.
Balozi Mbarouk ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 65 ya Uimamu wa Kiongozi wa Kiroho wa Madhehebu ya Shia Ismailia duniani, Mhe. Karim Aga Khan.
Balozi Mbarouk ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Taasisi hiyo, amesema Taasisi hiyo ambayo kupitia miradi mbalimbali iliyopo Tanzania Bara na Zanzibar ikiwemo ya elimu na afya na ile ya kujikwamua kiuchumi imewasaidia watu wengi ambapo hadi sasa takriban watoto 10,000 nusu ya hao wakiwa wasichana wamefaidika kwa kupata elimu bora kupitia taasisi hiyo.
“Kupitia uongozi mzuri wa Mheshimiwa Aga Khan, Taasisi ya AKDN imekuwa mstari wa mbele kuchangia katika sekta za elimu, afya, maendeleo ya uchumi na kuondoa umaskini kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar. Hivyo ninayo furaha kuungana na jamii ya Ismailia ya hapa nchini na duniani kwa ujumla kusherehekea siku hii muhimu ya miaka 65 ya Mhe. Aga Khan kuwa Imam wa Madhehebu ya Shia Imailia” alisema Balozi Mbarouk.
Kadhalika, Mhe. Balozi Mbarouk alisema anapongeza jitihada zinazoendelea kufanywa na AKDN katika kuboresha huduma za afya nchini ambapo kupitia jitihada hizo, mwezi Aprili 2022, Mkuu wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii ya AKDN, Mhe. Zahra Aga Khan, Mkuu wa Kamati ya Jamii ya AKDN alitembelea Tanzania na kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Kituo cha Huduma za Saratani jijini Dar es Salaam cha kiwango cha kimataifa ambacho kitakuwa na uwezo wa kutoa huduma mbalimbali kuhusu ugonjwa wa saratani ikiwemo kinga, utambuzi wa mapema wa ugonjwa, matibabu na huduma za nyumbani kwa wagonjwa .
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa Taasisi ya AKDN hapa nchini, Mhe. Balozi Amin Kurji amesema Taasisi yake itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia sekta mbalimbali zikiwemo za afya na elimu. Amesema, kupitia taasisi hiyo tayari miradi mbalimbali ikiwemo ya Vyuo Vikuu, Vyuo vya Afya vya wauguzi na wakunga vimeanzishwa nchini.
Aidha, ameishukuru na kuipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maendeleo makubwa ya uchumi na jamii yaliyopatikana nchini katika kipindi kifupi tangu aingie madarakani na kwamba Taasisi ya AKDN itaendelea kushirikiana na Serikali ili kuunga mkono jitihada hizo.
“Nampongeza Mhe. Rais Samia na Serikali yake kwa ujumla. Tumeshuhudia uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuboresha sekta za afya, elimu maji, umeme, miundombinu na sekta za uzalishaji. AKDN inaahidi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha maisha ya Watanzania” alisisitiza Balozi Kurji.
Maadhimisho hayo ambayo yalifanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam yalihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, Mabalozi, Wabunge na Wageni wengine waalikwa.
from MPEKUZI
Comments
Post a Comment